RC MAKALLA:WADAU WA MICHEZO TUUNGANISHE NGUVU ILI PAMBA JIJI FC ITIMIZE LENGO LA KUCHEZA LIGI KUU MSIMU UJAO
*Ayaomba Makampuni Mkoani Mwanza kuwekeza kwa Pamba Jiji FC*
*Asema timu ipo katika mazingira mazuri hivi sasa kinachohitajika ni nguvu ya pamoja ili kufikia malengo*
*Awataka wachezaji kutanguliza nidhamu na kujituma uwanjani*
Wakati kipenga cha Ligi ya Championship kinatarajiwa kupulizwa mwanzoni mwa mwezi ujao, wadau wa michezo Mkoani Mwanza wameombwa kujitokeza kuipa nguvu timu hiyo ili malengo ya kucheza Ligi kuu msimu ujao yatimie.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.CPA Amos Makalla ametoa kauli hiyo leo kwenye uwanja mkongwe wa Nyamagana mara baada ya kuitembelea mazoezini na kuzungumza na wachezaji na uongozi wa timu hiyo,Makalla amesema Pamba Jiji FC sasa ipo katika mazingira mazuri hivyo kinachohitajika na kuunganisha nguvu kwa kila mwenye uwezo wa kuichangia chochote.
Makalla ambaye pia ni mlezi wa wana TP LINDANDA kama inavyojulikana na mashabiki wake,amebainisha male go ya kupanda Ligi kuu yanakwenda na mshikamano wa pamoja huku timu ikiwa tayari imeimarishwa.
"Nitoe wito kwa wana Mwanza wote hii ni timu yao ambayo sasa ipo chini ya Halmashauri yetu ya Jiji,umoja wetu wa kila mwenye uwezo kuichangia itaongeza ari kwa wachezaji wetu na mwishowe kupata burudani ya Ligi kuu,tuna viwanja viwili vyenye ubora Nyamagana na Kirumba tuna kila sababu ya kufikia malengo yetu," Makalla.
Makalla ambaye ameupiga mpira miaka ya nyuma amewataka wachezaji kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa kuonesha bidii dimbani na kutanguliza nidhamu kwa ujumla.
"Wote tuna Imani kuwa Pamba Jiji FC ipo katika mikono salama hasa baada ya kuimarisha dawati la ufundi kwa kuwa na kocha mahiri Mbwana Makatta,"CPA Makalla.
Mara baada ya mazungumzo na wachezaji hao,mlezi wa timu hiyo aliwapatia motisha ya Shs 1000,000 iliyoungwa mkono na Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mwanza,MZFA Vedasto Lufano aliyetoa kiasi kama hicho.
"Mhe.Mkuu wa Mkoa tumepokea maagizo yako yote na tutahakikisha tunafikia malengo ya kucheza Ligi kuu msimu ujao,tunafarijika tuna timu nzuri na inaendelea kuimarishwa,"Sima Costantine Sima,Meya wa Jiji
"Tunaendelea kukushukuru mlezi wetu kwa nia ya dhati unayoendelea kuionesha kwa timu ya Pamba Jiji FC kama ulivyowatembelea leo wachezaji hii inazidi kuwapa ari ya kufanya vizuri,"Vedasto Lufano,M/kiti MZFA.
"Timu hivi sasa Ina mchanganyiko wa wachezaji wazawa na baadhi waliotoka nje ya Mwanza,tunaendelea kufanya mazoezi na mchujo ili tuje kupata kikosi imara kitakachoweza kumudu kishindo cha Ligi ya Championship,"Mbwana Makatta,Kocha Mkuu Pamba Jiji FC
Akitoa shukrani kwa niaba ya wachezaji wenzake,Jerryson Tegete amebainisha wamefarijika kutembelewa na mlezi wao hivyo wao wanawaahidi Mwanza kutowaangusha lengo la kucheza Ligi kuu msimu ujao.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.