Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Adam Malima amewataka viongozi na wataalamu wanaotoa elimu ya mfumo wa manunuzi ya Pamba kidijitali kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wadau wote ili kuondokana na malalamiko mbalimbali ya wakulima kuhusu kupunjwa uzito,wizi na kucheleweshewa fedha za malipo.
Mhe.Malima ameyasema hayo mara baada ya kufungua kikao hicho na kusema kuwa mfumo wa kidijitali kwenye shughuli za kilimo unaenda kuongeza usimamizi, ufanisi na upatikanaji wa takwimu sahihi kwa ajili ya mpango wa bajeti na uendelezaji wa sekta ya kilimo.
"Wakati tunaenda kuhamasisha matumizi ya mfumo huu wa kidijitali ni muhimu kuendelea kutoa elimu kwa wakulima, viongozi wa vyama vya ushirika, Serikali za mitaa na wataalamu wa kilimo na wadau wa pamba ili kujenga uelewa wa pamoja na uwezo wa matumizi ya vifaa mbalimbali vya kidijitali," amesema Mhe.Malima.
Mifumo hii inakwenda sambamba na kurahisisha malipo ya fedha kwa wakati kwa wadau mbalimbali hivyo ni hamasa kwa wakulima kufungua akaunti ili kurahisisha malipo kufanyika kwa wakati, amesisitiza.
Naye Mkaguzi wa Pamba wa Kanda ya Magharibi (TCB) Bw.Ally Mabrouke amesema kuwa kinachofanyika ni kurahisisha utaratibu uliokuwa ukitumika awali,ambapo kwa sasa zilizile taratibu zimerahisishwa na kuwekwa katika mfumo mmoja,na kusikiliza kuwa badala ya kutumia makaratasi kila kitu kitakuwa kwenye mfumo rasmi uliorahisishwa.
Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha Ushirika Shinyanga (SHIRECU) Kwiyolecha Nkilijiwa amesema anatamani Mkulima wa pamba ajivunie kilimo hiki kwani kwa sasa hawawezi hata kujenga nyumba nzuri ,na kusisitiza kuwa mfano huo utakapoanza kutumika inaonekana utamsaidia mkulima kwa kupata manufaa katika kazi yake.
Mhe. Malima ameongeza kuwa kwa msimu wa mwaka 2022/2023 uzalishaji wa pamba ulikuwa ni kilogramu 15,948,790 zenye thamani ya 26,688,226,722 kwa msimu ujao wa mwaka 2023/2024 Mkoa umelenga kuzalisha na kuuza kilogramu za pamba ghafi zipatazo kilo 56,007.12 na kupelekea matarajio ya zao la pamba kuongezeka kila mwaka kutokana na mpango wa Serikali katika kuinua Sekta ya Kilimo hususani mpango huu mpya wa mauzo ya Pamba kidijitali.
Kikao cha kujadili mfumo mpya wa mauzo ya Pamba kwa njia ya kidijitali kimefanyika katika ukumbi wa Kipepeo Mwanza Hoteli na kujumuisha wanunuzi wa zao la pamba, Bodi ya Pamba Tanzania, Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Bodi ya Usimamizi wa stakabadhi za ghala na soko la bidhaa Tanzania.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.