Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima ametoa rai kwa benki ya NMB kuendelea kuchangia maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi nchini kupitia huduma za kifedha wanazotoa.
Akizungumza na Viongozi na Mameneja wa benki hiyo waliotoka kanda zote nchini leo Jijini Mwanza, Mhe. Malima amewapongeza kwa kubuni huduma mpya bora za kiushindani wanazozitoa kwa jamii kama zinazowanufaisha wajasiliamali wadogo.
Aidha, Mhe. Malima ameipongeza benki hiyo kwa kuendelea kuboresha huduma zao kwenda kwenye mifumo ya kidigiti siku hadi siku kwani kwa maendeleo ya sayansi na teknolojia jambo hilo haliepukiki kutokana na ushindani wa kibenki.
"Faraja yangu kubwa kwenu ni kuona mnajihusisha na Sekta ya Kilimo tena katika nyanja zote za mifugo, uvuvi na ufugaji wa Nyuki sehemu ambazo wananchi wengi wanaendesha maisha yao huko" Amesisitiza Mkuu wa Mkoa.
Vilevile, ametoa wito kwa benki hiyo kuborsha huduma za mikopo kwa wajasiliamali na vikundi vya wananchi wanaojihusisha na shughuli ndogondogo za kujitafutia kipato kwa kuweka masharti mepesi kwani wananchi wengi wa kipato cha chini lakini wamekua wakikosa mitaji.
Mwenyekiti wa Bodi ya NMB, Dkt. Edwin Mhede amesema Benki hiyo ina mikakati ya kuwafikia wananchi kupitia uwajibikaji wao kwa jamii kwa kuwa sehemu ya Maendeleo yao kwa kuiunga Mkono Serikali kusaidia kwenye utoaji wa huduma mbalimbali kwa kusaidia vifaa kwenye Sekta ya Maji, Elimu na Afya.
"Benki yetu ilianzishwa mwaka 1997 na wakati huo tulikua na Matawi 97 tu nchini lakini sasa tumefikisha 228, tulikua hatuna mifumo ya digitali lakini hivi sasa tuna mifumo mbalimbali na tunashukuru sana Serikali, Wadau na Wateja wetu kwani wametupa faida kubwa hadi kufikia Bilioni 321 baada ya kodi ndani ya robo tatu tu za Mwaka." Kaimu Mtendaji Mkuu NMB, Filbert Mponzi.
Mkutano huo wa Benki ya NMB umewakutanisha Viongozi na Mameneja zaidi ya 250 kutoka kanda zote nchini wakisherehekea kwa pamoja kuwa na tuzo 18 ndani ya mwaka mmoja kwa utoaji wa huduma mbalimbali kwa ubora mkubwa kutokana na kufanya Biasha kwa ufanisi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.