Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe Adam Malima amewataka washiriki wa maonesho ya Biashara ya Afrika Mashariki kutumia fursa hiyo kuonesha bidhaa zenye ubora wa hali ya juu na zenye viwango thabiti ili kuupa hadhi inayostahili Mkoa huo.
Mhe Malima ametoa rai hiyo Agosti 29, 2022 wakati akifungua Maonesho ya Biashara ya Afrika Mashariki yanayofanyika kwenye viwanja vya Nyamagana mjini mwanza wakati akizungumza na wananchi na washiriki wa maonesho hayo.
"Wito wangu kwenu TCCIA na wadau wengine wa maonesho haya ni kwamba tufanye mambo haya kwa ufanisi mkubwa na mtu akija hapa akutane na maonesho makubwa yenye hadhi ya Mkoa wa mwanza yaani mambo yetu yawe na hadhi na taswira ya mkoa mkubwa wa pili nchini kwenye masuala ya kibiashara." amesema Mkuu wa Mkoa.
Katika kuyaboresha maonesho hayo, Mhe. Malima ametoa rai kwa TCCIA kuainisha maeneo bora zaidi ya kufanyia maonesho ili kwa kushirikiana na ofisi za wakuu wa wilaya maonesho ya mwaka 2023 yafanyike kwenye eneo rasmi lenye hadhi na sio kwenye uwanja wa mpira.
Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Mwanza, ndugu Gabriel Kenene amesema pamoja na mambo mengine chemba hiyo inawaunganisha wafanyabiashara na wakulima na kuwawezesha kupata mazingira bora ya uwekezaji kwenye masuala ya Uwekezaji nchini.
Vilevile, bwana Kenene amebainisha changamoto kadhaa zinazowakabili zikiwemo kutokuwepo kwa sera ya viwanda na biashara na sekta binafsi ya kutatua changamoto zinazoikabili sekta binafsi nchini na akatoa rai kwa serikali kutatua changamoto zinazoikabili sekta binafsi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.