Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima amewataka wasimamizi wa Mradi wa Ujenzi wa jengo la kisasa la abiria kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwanza kusimamia kwa dhati na wawe na kiu ya kuukamilisha kwa wakati ili uanze kutumika.
Mhe. Malima amesema hayo leo wakati wa Kikao Kazi cha kujadili Mapendekezo Mapya ya Usanifu wa baadhi ya maeneo kwenye Jengo jipya la Abiria kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwanza ambapo amebainisha kuwa litakapokamilika jengo hilo la kisasa litasaidia kuinua uchumi kwenye ukanda huo.
"Ninachokitaka kwenu nyie Wahandisi, msimamie kwa uzalendo ujenzi huu na kila mmoja wetu hapa awe na lengo la kuukamilisha maana mradi huu ni wetu sote na utainua sana utalii wa nchi hasa kwenye ukanda wa kanda ya ziwa." Malima.
Amesema, Mkoa wa Mwanza unawekeza kwenye majengo hayo kwa kupitia Halmashauri za Manispaa ya Ilemela na Nyamagana zilizotoa fedha Tshs. Bilioni 4 za mapato ya ndani kwenye ujenzi huo na amewasihi kuongeza fedha ili likamilike na amefafanua kuwa litakapokamilika utawekwa utaratibu wa kuwa wadau wa uwekezaji ili kiasi fulani cha fedha zirudi kwenye Halmashauri hizo.
Katika kuimarisha uchumi wa Mwanza kupitia sekta ya Utalii, Malima ametoa mfano wa uzao wa Nyumbu unaofanyika kila mwaka mwezi februari kwenye hifadhi ya Serengeti kuwa jengo hilo litakapokamilika litatumika kwakua litakua maridadi na nadhifu kwa viwango vya ndani na nje ya nchi.
Mhe. Malima amesisitiza uzalendo kwenye ujenzi huo kwa kuzingatia bei ya manunuzi ya vifaa na kusimamia ubora wa jengo ili liweze kudumu kwa muda mrefu na kuwanufaisha wanachi wa mikoa ya kanda ya ziwa na Taifa kwa ujumla.
Ndugu Balandya Elikana, Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza amesema kutokana na umuhimu wa Ujenzi wa jengo hilo Ofisi yake itasaidia kutoa ushauri wa namna ya kufanikisha kwa kufanya mapitio kwenye bajeti inayoendelea kutekelezwa na Halmashauri hizo mbili na kwa kuangalia vipaumbele Ujenzi huo utawezekana.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.