Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Afya kuona namna ya kujenga Hospitali ya Rufaa ingine mkoani humo ili kuondoa msongamano kwenye hospitali za Bugando na Sekou Toure kutokana na ongezeko kubwa la watu kanda ya ziwa.
Amebainisha hayo leo alhamisi (Januari 05, 2023) wakati akifunga kikao cha wadau wa Afya kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mkuu wa Mkoa kilichoongozwa na Prof. Abel Makubi Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya wakati akihitimisha ziara ya Utoaji Elimu kuhusiana na muswada wa bima ya Afya kwa wote unaokwenda kujadiliwa bungeni siku za usoni.
Ameongeza kuwa katika kuboresha huduma za magonjwa ya Saratani Uongozi wa Mkoa umepeleka mapendekezo kwa Wizara ya afya kukipandisha hadhi kitengo cha kuhudumia magonjwa ya Saratani kwenye Hospitali ya Kanda Bugando kuwa hospitali kamili kutokana na waathirika wengi wa tatizo hilo wanatoka kanda ya ziwa.
Vilevile, amesema Mkoa umeiomba wizara kuleta Madaktari Bingwa kwenye Hospitali inayojengwa Wilayani Ukerewe kwa hadhi ya Rufaa ya Mkoa kuhakikisha vifaa tiba na wataalamu wapatikana ili wananchi waishio visiwani wapate huduma za kibingwa wilayani Ukerewe.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amesema Serikali iko mbioni kuboresha huduma za afya kwenye kitengo cha Saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando na ukamilishaji wa haraka utafanyika kwenye Hospitali yenye hadhi ya Rufaa ya Mkoa inayojengwa Nansio-Ukerewe.
"Nia ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya jirani na kwenye makazi yao, hivyo tunakwenda kuboresha huduma za Saratani Bugando maana kwa sasa pale kuna mashine moja ambayo haitoshi" Amesisitiza Prof. Makubi.
Aidha, amesema Wizara ya Afya inaendelea kutoa Elimu ya Bima ya Afya kwa wote kwa wananchi kuanzia ngazi za kitongoji hadi Taifa ili kuhakikisha wananchi wote wanapata uelewa wa suala hilo ambalo siku za karibuni litafikishwa bungeni kwa ajili ya kupata muswada ambao baadae utakua sheria rasmi.
Prof. Makubi ametoa rai kwa viongozi nchini kushirikiana na wizara hiyo katika kutoa Elimu na amewataka kuwa mbegu bora itakayofikisha Elimu ngazi za chini kupitia wadau na wataalamu wa afya nchini kwa kushirikiana na wana habari na kwamba mpango huu utakua na gharama za chini zaidi ya hali ilivyo kwenye bima za sasa.
Mjumbe wa Sekretarieti ya Bima ya Afya kwa Wote nchini, Bi. Jackine Tarimo amesema Chimbuko la kuanzishwa kwa muswada huo ni kutimiza wajibu wa Serikali kikatiba wa kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya bila kikwazo.
"Uhalisia unaonesha kuwa na idadi kubwa ya wananchi (asilimia 85) hawana bima za afya na hivyo kukosa uhakika wa kupata huduma za afya pindi zinapohitajika lakini kwa muswada huu utaonesha kuwa wananchi wote hasa wasio na uwezo watapata fursa ya kuingia kwenye huduma za Bima." Amesema Tarimo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.