Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima amekabidhi Baiskeli 70 na Fimbo 30 kwa watu wenye mahitaji maalum vilivyotolewa na Mhe. Furaha Matondo Mbunge wa Viti Maalum Mkoani Mwanza kutoka Jimbo la Ukerewe Mkoani humo.
Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi Vifaa hivyo iliyofanyika mapema leo Jijini Mwanza, Mhe. Malima amekemea tabia ya Unyanyapaa inayofanywa na baadhi ya watu kwa watu wenye Ulemavu na badala yake amewataka kuwapa nafasi ya kushiriki kujenga nchi katika vitu tofauti ambavyo wana vipaji navyo.
Vilevile, amemshukuru Mhe. Matondo kwa msaada huo na amemtia moyo kuendelea kuwajali wenye Ulemavu na akatoa wito kwa wengine kujitoa kwa kundi hilo muhimu na kwamba kwa Mwenyezi Mungu amefanya hisani yenye Ibada ndani yake.
Aidha, amewakemea wazazi na viongozi wanaonyamazia matukio ya ukatili wa kijinsia yanayotokea kwenye jamii na akawataka kuona kama ni jukumu la kila mmoja kukemea matendo kama ya ulawiti, ukatili na Unyanyasaji wa jamii ili kutokomeza madhira hayo kwenye jamii.
"Watoto wananyanyaswa sana, ulawiti na ubakaji vimekithiri sana nami nimehuzunishwa sana na matukio ya ukatili wa kijinsia na kwa watoto wadogo alafu jamii inawajua waovu hawa kwakuwa wanaishi nao" Ameongea Mhe. Malima wakati akionya kuhusiana na Ukatili wa kijinsia.
Mhe. Jamal Babu Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa akiwakilisha Mkoa wa Mwanza ametoa wito kwa Serikali kuendelea kuwajali watu wenye ulemavu nchini kwa kuwapa kipaumbele kwenye huduma na kuwawekea Miundombinu rafiki kwa matumizi hususani kwenye Shule na Zahanati.
Naye Mhe. Furaha Matondo amesema anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumjalia kupata vifaa hivyo na kusaidia watu wenye uhitaji na hiyo yote amefanya kwa moyo wa dhati ikiwa ni kumsaidia Mhe. Rais katika kuboresha maisha kwa makundi ya watu wenye Ulemavu.
Bi. Neofita Mkiringi, Mtaalamu wa Viti Mwendo kutoka CCBRT ametoa wito kwa viongozi wanaotaka kutoa misaada ya Viti Mwendo kuwashirikisha wataalam wa Magonjwa ya viungo kabla ya kufanya hivyo ili kuwalinda watumiaji na matatizo ya vidonda Mkandamizo, Mgongo kupinda na miguu kuumia.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.