Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe Adam Malima Jumanne hii ametoa wiki sita kwa Mkandarasi anayejenga barabara ya lami ya kilomita mbili ya Nakutunguru na Nkilizya mjini Nansio kutokana na kusuasua kukamilisha kwa wakati.
Mhe Malima katika ziara yake ya kujitambulisha Wilayani humo na kukagua Miradi ya maendeleo,amesema barabara hiyo ya zaidi ya Shs milioni mia tisa imeanza kuwa mzigo kwa wananchi ambao wamemlalamikia tangu ameingia Wilayani humo.
"Nasema wazi katika hili sina mzaha huyu Mkandarasi mwezi ujao nitakuja hapa asipokamilisha nitajua la kufanya" Mkuu wa Mkoa
Mhe Malima katika ziara hiyo amefanya ukaguzi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya mjini Nansio yenye gharama ya zaidi ya Shs Bilioni 2 ambayo sasa imesimama kutokana na utata wa gharama halisi,Chuo cha Veta kilichopo Muhula,Shule ya Sekondari iliyopo Kagunguli na Kituo cha Afya cha Igalla
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa katika mazungumzo na Watumishi wa Halmashauri amewahakikishia kuitazama Wilaya ya Ukerewe kwa jicho la tatu akimaanisha kuiinua kimapato hasa kutokana na kuzungukwa na fursa za Uchumi wa bluu.
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Mhe Dennis Mwila amesema wanaishukuru Serikali ya awamu ya Sita kwa kuleta Miradi mingi Wilayani humo ikiwemo ya afya,elimu na maji ambayo imekuwa na tija kwa wananchi.
Amemuomba Mkuu wa Mkoa kuingilia kati na kuipatia ufumbuzi kwa baadhi ya Miradi ambayo imegunikwa na ubabaishaji na kuwa mzigo kwa wananchi.
Mkuu wa Mkoa Mhe Adam Malima amekamilisha ziara za kujitambulisha na kukagua Miradi ya Maendeleo wilaya zote za Mkoa wa Mwanza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.