Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima amekabidhiwa mtambo wa kisasa wa kuchimba Visima na Malambo yenye thamani ya Shs milioni 550 ambayo itaanza kuchimba Visima 83 kwenye baadhi ya maeneo Mkoani humo.
Akizungumza katika hafla fupi ya kuwakabidhi mitambo hiyo kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) iliyofanyika Wilayani Misungwi, Mhe.Malima amesema licha ya Mkoa wa Mwanza kuwa na rasilimali kubwa ya maji ya Ziwa Victoria lakini kuna baadhi ya maeneo wananchi hawapati huduma hiyo hivyo mtambo huo ni ukombozi wa kumtua ndoo kichwani mwanamke.
"Kwa niaba ya wananchi wa Mwanza natoa shukran kwa Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ameonesha upendo wa dhati wa kuendelea kuwapigania maendeleo wananchi wake,nawaomba sana tuitunze na tuitumie kwa malengo yaliyokusudiwa mitambo hii".Amesisitiza Mkuu huyo wa Mkoa.
"Mhe.Mkuu wa Mkoa bado tunaendelea kupambana kuhakikisha huduma ya maji vijijini tunafikia asilimia 85 na mijini 95 hadi kufika mwaka 2025 kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi inavyotutaka".Mhandisi Godfrey Sanga.Meneja RUWASA Mkoa
Amesema uchimbaji wa Visima 83 kwa bei ya Mkandarasi ingefikia Shs.2,554,265,406 lakini kwa kutumia mitambo hii wanatarajia kutumia Shs.2,118,575,000 hivyo wameokoa Shs.435,690,406.
Mitambo hiyo ya kuchimba Visima imesambazwa Mikoa yote 25 ya Tanzania Bara iliyogharimu zaidi ya Shs Bilioni 15.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa akiwa njiani kwenda kukagua miradi ya maji huko Ihelele Wilayani Misungwi amepita kwenye shamba la Uzalishaji Mifugo la Mabuki na kutoa maelekezo kwa Maafisa Mifugo wote kutoka Halmashauri kukutana kwa ajili ya kuweka mkakati wa kujifunza namna ya ufugaji wenye tija wa kuwa na Mifugo michache yenye ubora na kumuingizia kipato mkulima.
"Nimepita hapa nami kuna somo nimelipata ambalo ni lazima wasaidizi wangu waje hapa kujifunza ili wakamsaidie mfugaji namna ya kujiongezea kipato kwa ufugaji wa kisasa".Amesema Mhe.Malima.
"Shule hii ya Sekondari ya wasichana ya Mwanangwa inayojengwa na TASAF, naendelea kusisitiza Miradi hii yote iwe imekamilika mwishoni mwa Machi mwaka huu kama tulivyoahidi kwa Waziri Mhagama kuwa tutamaliza Miradi yote ya TASAF kabla ya Aprili hasa baada ya kuonesha kuwa nyuma kukamilisha Miradi mingi licha ya fedha kutolewa zote na kuwa hatarini Mkoa wetu kukosa fedha nyingine awamu ijayo ya TASAF" Amehimiza Mhe. Malima alipopita kukagua shule hiyo itakayoanza Januari mwakani.
TASAF imetoa jumla ya Shs milioni 683,005,234.74 kukamilisha mradi wa shule hiyo.
Akiwa kata ya Nyamahiza kusikiliza kero za Wananchi, Mkuu huyo wa Mkoa ameiagiza RUWASA na TANESCO kuwaharakishia Maendeleo wananchi kwa kuwaletea huduma haraka na kuwataka walimu wa shule ya Sekondari Magufuli kufuata taratibu za Utumishi wa umma baada ya kupata taarifa za kuwepo upungufu wa walimu ambao wameondoka huku wakitoa visingizio visivyo na tija.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.