*RC Malima asaini Mkataba wa lishe baina yake na Wahe.Wakuu wa Wilaya*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Adam Malima leo Octoba 28 ameongoza zoezi la utiaji saini wa Mikataba ya Afua za Lishe baina yake na Wahe. Wakuu wa Wilaya saba zilizopo mkoani humo.
Akizungumza kabla ya kutia saini mikataba hiyo, Mhe.Malima amewataka Wahe.Wakuu wa Wilaya hizo kuhakikisha wanaisoma na kuielewa ili waweze kuifanyia kazi kikamilifu kama ambavyo imekusudiwa na Serikali.
" Nawaombeni Wahe. Wakuu wa Wilaya isomeni na kuielewa siyo kuisoma tu kwa kuwa mkiielewa mtaifanyia kazi na matokeo tutayaona ila mkiisoma tu mtaiacha hapo hapo," amesema Mhe.Malima.
" Chakula cha Lishe hakitakiwi kuwa na gharama kubwa... sasa nawaambia Wahe.Wakuu wa Wilaya nendeni mkatoe Elimu ya Lishe ....na haina haja ya kutumia maneno magumu waelewesheni wananchi kwamba lishe siyo lazima iwe mayai, nyama na samaki wambieni lishe ni mboga za majani kama matembele, kunde, maharage vyote hivyo ni lishe" amesisitiza Mhe.Malima.
Aidha, ameongeza kuwa mikataba hiyo inashuka mwanzo ilikuwa kati ya Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan na Wakuu wa Mikoa na sasa ni Mkuu wa Mkoa na Wahe. Wakuu wa Wilaya na baadaye Wakurugenzi.
Hata hivyo, Mhe.Malima ameongeza kuwa Jambo kubwa katika mikataba ya Lishe ni Elimu juu ya Swala la lishe, kwa kuwa vitu vyote vinavyohusu Lishe vinapatikana katika mazingira ya wananchi.
"Wapeni Elimu wananchi juu ya matumizi ya vyakula hivyo ili viwaletee afya watoto wetu,"amesisitiza
Naye, Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt.Thomas Rutachunzibwa amesema mkataba huu ni wa msingi sana ukizingatia kuwa hali ya Udumavu iko juu takriban asilimia 29 katika mkoa wa Mwanza hivyo wameupokea Mkataba huo na kuahidi kuusimamia katika utekelezaji wake.
Kwa upande wake Bw.Daniel Machunda Katibu Tawala Msaidizi Utawala Mkoa wa Mwanza akimuwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa huo Balandya Elikana, awali akimkaribisha Mhe.Mkuu wa Mkoa amesema kikao hicho ni kufuatia agizo la Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kuwa ifikapo Oktoba 30 Mikataba yote ya Lishe iwe imesainiwa.
Kikao hiki kimefanyika kufuatia maelekezo ya kikao kazi yaliyotolewa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, na Maafisa Lishe walio katika Sekretarieti za Mkoa kilichofanyika Mwezi Septemba, 2022 Mkoani Dodoma kuhusu Afua za Lishe, ambapo Mhe.Rais alielekeza Ofisi ya Rais TAMISEMI Kupitia Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wilaya kusaini mikataba ya Utendaji kuhusu masuala ya Lishe kati ya Mkoa na Halmashauri zao zote.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.