Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe Adam Malima amewaahidi kuwapigania kuwa na Benki ya Taifa ya Ushirika Muungano wa Ushirika wa akiba na mikopo SCCULT ili kuwa na nguvu kubwa ya kiuchumi itakayomkomboa Mtanzania na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza leo Jijini Mwanza kwenye Viwanja vya Furahisha wakati wa kufunga Maadhimisho ya Kimataifa ya Ushirika wa akiba na mikopo,Mhe Malima amesema haoni kinachoshindikana kwa umoja huo kujichangisha na kupata bilioni 15 kama mtaji wa kuanzisha Benki kwa mujibu wa taratibu za Benki Kuu ya Tanzania,hasa baada ya kuona baadhi ya Taasisi kuwa na mitaji ya zaidi ya bilioni 3.
"Mimi ni mkereketwa wa Ushirika huu naomba kuwaahidi kuzungumza na Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu nia ya kuanzisha Benki na Serikali inunue pia hisa,naimani pasipo shaka mkuu wetu wa nchi atanielewa"
Amesema baada ya kuzungukia mabanda na kupata taarifa za Taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi amepata somo zuri la umuhimu wa kuwepo kwa Ushirika huo ambao ni jawabu la kumkomboa mwananchi kiuchumi.
Aidha amewashauri Viongozi wa muungano huo wa ushirika kuendelea kuwa na nidhamu nzuri ya fedha hali itakayo waongezea Imani kutoka kwa wanachama wao.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi Mrajisi wa Ushirika Tanzania Dktr Benson Ndiege amesema kwa mujibu wa takwimu ya mwaka 2018-2022 inaonesha Watanzania milioni 21 bado hawajafikiwa na huduma za kifedha wakati Duniani inafikia idadi ya watu Bilioni 1.4, hivyo fursa za Ushirika huo zina kila sababu ya kuchangamkiwa hapa nchini.
Maadhimisho hayo yalitanguliwa na wiki ya Ushirika iliyoanza Septemba 16 iliyowapa Wananchi wa Mwanza kupata taarifa za shughuli za Ushirika huo na faida zake.
Mkoa wa Mwanza utakuwa mwenyeji tena Kitaifa mwakani wa shughuli za Ushirika huku uboreshaji zaidi ukiahidiwa kuwepo
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.