Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima amewaalika wananchi waishio Mkoani humo na jirani kuitikia wito wa kupata vipimo vya magonjwa mbalimbali kwenye viwanja vya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou Toure kuanzia Disemba 05 -09, 2022.
Mhe. Malima amesema kwa siku zote hizo tano kutakua na Madaktari Bingwa kutoka Sekou Toure kwa kushirikiana na Hospitali ya Kanda ya Bugando ambapo watafanya vipimo bure kwa wananchi katika magonjwa mbalimbali kuanzia saa 2 asubuhi hadi 12 jioni.
Aidha, amesema wananchi watapata nafasi ya kuangaliwa afya zao na kupata ushauri wa kitaalamu dhidi ya Magonjwa mbalimbali na kwamba matibabu yatafanyika kwa gharama nafuu na bima mbalimbali za afya zitapokelewa kwa matibabu.
Vilevile, ametoa wito kwa wananchi kuwa na bima za afya kwani magonjwa hayabishi hodi na yanatokea wakati mtu hana fedha hivyo mwananchi akiwa na bima itamsaidia kupata huduma bora.
Hata hivyo, ametumia wasaa huo kutoa wito kwa wataalamu hao wa afya kutoa elimu kwa umma dhidi ya magonjwa mbalimbali hasa yanayowakabili zaidi wananchi wa kanda ya ziwa ili jamii iweze kubaini na kujikinga nayo.
"Kuanzia wiki ijayo kwa kushirikiana na hospitali ya Bugando, kwenye Hospitali yetu tutakua na kambi ya Madaktari bingwa kwa kada Mbalimbali ambao watatoa huduma kama za Upasuaji, Uzazi, Watoto, akina mama na watoto, Mionzi, Meno, macho, Damu, mfumo wa Chakula na afya ya akili hivyo nawakaribisha wananchi wote kufika kwa wingi kupata huduma." Dkt. Bahati Msaki, Mganga Mfawidhi Sekou Toure.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.