RC Malima awataka Wauguzi kuutumia Mkutano wao Mkuu kutatua changamoto zao
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Adam Malima amewataka Wauguzi wanaoshiriki Mkutano wao Mkuu wa Chama cha Wauguzi nchini,TANNA unaofanyika Mkoani humo kuutumia kikamilifu kutatua changamoto zao ili kuboresha mazingira yao ya kazi.
Alifungua leo Mkutano huo wa 50 wa Chama hicho kwenye ukumbi wa Malaika Resort uliopo Jijini Mwanza,Mkuu huyo wa Mkoa amesema Wauguzi ni nguzo muhimu kwenye Sekta ya afya licha ya kukabiliwa na mazingira magumu na hatarishi katika kazi zao,hivyo Mkutano huo ndiyo jukwaa la kupaza sauti ili kasoro zilipo zifanyiwe kazi.
"Mmefanya uamuzi wa busara kuuleta Mkutano huu wa Kitaifa Mkoani Mwanza,niwasihi sana msikae hapa kwa siku tano na kuuchukulia kirahisi tu bali hakikisheni unakuja mageuzi chanya ili kuendelea kufanya kazi katika mazingira bora na salama",Amesisitiza Mhe.Malima.
Amesema Serikali ya awamu ya sita imezidi kuimarisha Sekta hiyo kwa kuhakikisha kunakuwepo na Hospitali na vituo vya afya vyenye ubora pamoja na upatikanaji wa dawa kwa wakati na hivi karibuni imetoa ajira 8070 kada ya afya.
"Mkutano huu tunaimani utakuja na matokeo chanya hasa kutokana na fursa za kuelimishana kupitia tafiti za kisayansi zilizofanyika,majadiliano na namna ya kuzitatua changamoto zinazotukabili yote ni baadhi ya faida kupitia Mkutano huu wa Kitaifa",Julius Shigella,Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Kwa upande wake Rais wa Chama cha Wauguzi nchini,Alexander Baluya amesema Mkutano huo umebeba mambo makuu matatu,Kongamano la Kisayansi lililoanza leo na kesho,Mkutano Mkuu wa 50 na siku ya Wauguzi Duniani inayoadhimishwa kila Mei 12 ambayo wataiadhimisha siku ya kufunga Mkutano huo.
"Mkoa wa Mwanza tuna jumla ya Wauguzi 4000 na vituo vya afya 600,licha ya uchache wetu na kuhudumia idadi kubwa ya wateja,lakini Wauguzi tumesimama imara kuhakikisha tunatoa huduma bora siku zote",Claudia Kaluli,Muuguzi Mkuu Mkoa wa Mwanza.
Mkutano huo uliobeba kauli mbiu ya WAUGUZI WETU,MUSTAKBARI WETU umewajumuisha washiriki 1200 wakiwemo Wauguzi wakuu kuanzia ngazi ya Mikoa na Wilaya.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.