Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mh.Adam Malima amemshukuru Rais Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuonesha kwa vitendo Miradi ya kuwainua wananchi kiuchumi na kuwaahidi wakazi wa Sengerema ulinzi na usalama wa Miradi iliyosainiwa leo ya Barabara ya Sengerema-Nyehunge ya KM 54.4 na Kivuko cha Buyagu-Mbalika.
Akimkaribisha Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi,Mhe.Mhandisi Godfrey Kasekenya kwenye hafla ya utiaji saini wa Miradi hiyo kwenye viwanja vya mnadani Wilayani Sengerema,Mhe.Malima amesema hayupo tayari kushuhudia uhujumu uchumi kwenye Miradi hiyo kwa kufanyika udokozi wa aina yoyote wakati Serikali ya Rais Samia ikiwa mstari wa mbele kuwapigania maendeleo wananchi wake.
"Leo tumeshuhudia muendelezo wa miradi mingi hapa Mkoani kwetu,huu wa Barabara umegharimu zaidi ya Shs Bilioni 73 na wa Kivuko zaidi ya Shs Bilioni 3 ni lazima tuoneshe umakini kwenye Miradi hii yenye tija kwa wananchi".Amesisitiza Mkuu huyo wa Mkoa
Aidha amewakumbusha Wakandarasi walioshinda zabuni hizo kuwa na weledi katika kazi zao ziwe na ubora na kukamalisha kwa wakati miradi hiyo ili kuharakisha maendeleo ya wananchi.
"Nawapongeza sana Wabunge wa Mkoa wa Mwanza,Mhe.Eric Shigongo wa Buchosa,Mhe.Alexander Mnyeti wa Misungwi na Mhe.Hamis Tabasamu wa Sengerema mnafanya kazi kubwa ya kuwapigania maendeleo wananchi wenu hali ambayo nami mnanirahisishia kwa kiwango kikubwa,asanteni sana".Mhe.Malima.
"Kwa mwaka huu tuna jumla ya Vivuko vipya 6 vilivyo gharimu Sh Bilioni 33.2 na vya ukarabati vipo 18 vilivyogharimu Shs Bilioni27.5,hii inaonesha ni jinsi gani Serikali ya awamu ya Sita ilivyoweka kipaumbele uimarishaji wa miundombinu ambayo ni nguzo muhimu wa uchumi wa nchi"Mhe.Mhandisi Godfrey Kasekenya,Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi.
Akizungumzia ujenzi wa barabara hiyo Mbunge wa Sengerema Mhe.Hamis Tabasamu amesema kwa muda mrefu shughuli za kiuchumi kuanzia za mazao ya Uvuvi na kilimo zilizorota kutokana na hali mbaya ya miundombinu ya barabara,lakini kwa ujenzi huo sasa utakuwa na tija pia kwa Halmashauri za Sengerema na Buchosa.
"Mheshimiwa Naibu Waziri Kasekenya nakupongeza kwa hatua hii,lakini jimboni kwangu barabara ya Mwanangwa-Misasi hadi Kahama mwaka huu usiponiwekea kiwango cha lami sitakuelewa nimeizungumzia kwa muda mrefu sana kutokana na umuhimu wake."Mhe Alexander Mnyeti Mbunge wa Misungwi.
"Binafsi namshukuru sana Mhe.Rais Jimbo langu asilimia kubwa wakazi wake wapo visiwani,kuimarishiwa barabara hii ni ukombozi kwao hasa katika shughuli zao za Uvuvi kwani watakuwa wanafanya kazi zao kwa uhakika".Mhe.Eric Shigongo,Mbunge wa Buchosa.
Utiaji huo wa saini kwa upande wa barabara umewahusisha Mtendaji Mkuu wa Tanroad nchini Mhandisi Rogatus Mativila na Mkandarasi AVM Construction kutoka Uturuki na upande w Kivuko alikuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa ufundi na umeme TEMESA, Mhandisi Lazaro Kilahala na Mkandarasi Songoro Marine.
Kwa mujibu wa mikataba hiyo Ujenzi wa barabara utachukua muda wa miaka miwili na miezi minne na Kivuko ni miezi kumi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.