Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima amekabidhi Vifaa vyenye thamani ya zaidi ya Milioni 104 kwa Vikundi vya vijana wajasiriamali 168 vilivyotolewa na Shirika la Plan International baada ya kuhitimu na kufuzu mafunzo katika fani mbalimbali tayari kwenda kujitafutia kipato.
Akizungumza na vijana hao waliohitimu mafunzo chini ya mradi wa 'Vijana, Maisha na Kazi' katika hafla ya Kukabidhi vifaa iliyofanyika leo Agosti 18, 2022 kwenye viwanja vya Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Mwanza, Mhe. Malima ametoa wito kwa wahitimu kuyatumia mafunzo hayo kwa weledi na bidii kubwa katika kujitafutia ridhki kwa ustawi wa familia zao.
"Hakuna malipo ya wema kama si kufanya wema wenyewe, mradi huu wema wake ni kwamba umetoa Elimu na Ujuzi ambao vijana hawa wamepata na hakuna mtu anaweza kuwanyang'anya hata kama mtu akipoteza Cheti za ujuzi huo, tunawashukuru sana wadau wetu." Mhe. Malima.
Vilevile, Mkuu wa mkoa amekemea tabia ya kunyanyapaa watu wenye ulemavu huku akibainisha kuwa kuzaliwa na ulemavu sio laana bali ni majaaliwa ya mwenyezi Mungu na wanapaswa kupata nafasi kwenye kila kitu kama ambavyo wadau wa mafunzo hao walivyowapatia fursa ya kupata Ujuzi na Vifaa hivyo.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe. Hassan Masala ametoa pongeza kwa Shirika la Plan International, VETA na Wadau wengine wanaosaidia Serikali katika juhudi za kusaidia kutimiza malengo ya maendeleo kwa wananchi wake.
Mkurugenzi wa VETA kanda ya Ziwa Charles Kangele amewashukuru shirika la Plan International na ametumia wasaa huo kuwakaribisha wananchi kupata ujuzi na mafunzo stadi kwenye fani 11 zinazotolewa na Chuo cha VETA Mwanza na akabainisha kuwa Wilaya za Kwimba na Ukerewe wako mbioni kupata Vyuo vipya.
Meneja wa Shirika la Plan International wa Mikoa ya Mwanza na Mara Bwana Rwambali Majani amesema vijana 168 wamefuzu mafunzo kwa kushirikiana na VETA na wadau wengine katika fani za Ushonaji, Uchomeleaji, Ufundi Magari, Umeme wa Magari, Kutengeneza bidhaa za Almanium na Mabomba.
"Tunakabidhi vifaa vyenye thamani ya zaidi ya Milioni 104 ambavyo vitawasaidia katika kuzalisha kwa ustawi wa maisha yao wenyewe na ujenzi wa Taifa kwa Ujumla na mradi huu unafanya kazi kwenye kata 11 na kwa kushirikiana na SIDO, TAHA, VETA na SEDIT na tumewawezesha kwa gharama za mafunzo, usafiri na gharama za kulea watoto kwa waliojifungua wakiwa kwenye mafunzo." Amesema Majani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.