Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima amewahimiza Wananchi wa Mkoa huo kuendelea kuchukua tahadhari kuhusiana na ugonjwa wa Ebola pasipo kutishana ili kuondoa taharuki kwenye Jamii.
Akizungumza leo na wawakilishi wa makundi mbalimbali kuhusiana na utayari wa Mkoa wa Mwanza dhidi ya ugonjwa wa Ebola, Mhe. Malima amesema Elimu kwa jamii ndiyo njia sahihi ya kukabiliana na ugonjwa huo kama utaingia Mkoani humo.
"Niwasihi sana, kuanzia Viongozi wa Dini, Wataalamu wa Afya na Makundi mengine mliopo humu tupate uelewa mzuri kutoka kwa Wataalamu wanaotuelimisha leo humu ukumbini na tusione aibu kuuliza maswali ili tuwe mabalozi katika kuelimishana," amesema Mkuu wa Mkoa.
Malima ameongeza kuwa jamii ni lazima iendelee kuchukua tahadhari na kumuomba mwenyezi Mungu kuwaepusha na balaa hili hasa kutokana na ukaribu wa Mkoa wa Mwanza na Nchi ya Uganda ambako visa vya ugonjwa wa Ebola vimetokea na kuuwa watu kadhaa.
"Kama ikitokea mtu ameambukizwa tuepuke utamaduni tuliozoea wa kumhudumia mgonjwa kwa kugusana au maiti kuishika hiyo itachangia kuusambaza ugonjwa kwa kasi," amesema Dkt Rutachunzibwa wakati akitoa elimu ya tahadhari ya ugonjwa huo.
"Dalili za ugonjwa wa Ebola ni homa kali, kuhara na kutapika, kichwa kuuma sana, kutokwa na damu sehemu zote zenye matundu mwilini na kuishiwa na nguvu, hivyo unapomshuhudia mtu wa aina hii ni lazima kumuwahisha Hospitali haraka." Prof. Deodatus Kakoko, kutoka Chuo Kikuu kushiriki cha Afya Muhimbili.
Tayari Serikali imechukua tahadhari kupitia Mikoa yote hatarishi iliyopo Kanda ya Ziwa kuanzia sehemu za Bandari, Viwanja vya Ndege na sehemu za mipaka kwa kuweka Vifaa vya kisasa vya kubaini mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.