*RC Malima awaomba Viongozi wa Dini kuendelea kuliombea Taifa amani, kuepukana na Maradhi*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Adam Malima amewaomba Viongozi wa Kanisa la KKKT kuendelea kuisadia Serikali katika kuboresha hali za Kiuchumi na za Watanzania kwa ujumla kupitia huduma yao ya Lutheran Mission Corporation (LMC) ambayo lengo lake ni kuratibisha kazi za Umoja za KKKT.
Mhe.Malima ameyasema hayo leo Oktoba 6,2022 alipokuwa akihutubia mkutano wa Majumuisho wa Vyama 13 vya Kimisioni vya kanisa la Kiinjili la Kilutheli kutoka Nchi za Ulaya na Marekani ambapo Tanzania ni sehemu ya waliounda Shirikisho hilo la LMC uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Isamilo Jijini Mwanza.
Ameongeza kuwa, KKKT inaweza kushiriki katika kuwawezesha waumini kuunda vikundi mbalimbali vya uzalishaji na kuvisaidia kupata mitaji,kuwa na uongozi bora na kupata elimu ya biashara.
"Wahimizeni kufanya kazi kwa bidii na kwa maarifa wakati wote, wote mnakumbuka kuwa biblia Takatifu kwenye kitabu cha Wathesalonike: 3.10 inatueleza kuwa ikiwa mtu hataki kufanya kazi basi na asile,ni imani yangu kuwa waumini mmoja mmoja au katika vikundi wakiwa na nguvu kiuchumi, kanisa litakuwa na nguvu kiuchumi na vivyo hivyo kwa Serikali," amesema Mhe.Malima.
"Ninaamini kuwa viongozi wa dini mna mchango wenu mkubwa sana katika kuishauri Serikali na kueneza amani katika nchi yetu," ameongeza.
Aidha,Amesiaitiza kuwa, KKKT imeendelea kuwajenga na kuwasadia watanzania kiroho na kimwili kwa kuwawezesha kupata maji safi na salama, elimu na huduma za afya.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania Mhe. Dkt. Frederick Shoo amesema anaishukuru Serikali kwa ushirikiano mkubwa kwa kanisa, kwani wamekuwa mchango mkubwa hasa katika madhehebu ya Dini ikiwa ni pamoja na KKKT.
"Mhe Mkuu wa Mkoa kwa kukubali kutenga muda wako katika ratiba iliyonayo kwako wewe kutenga muda wako kwa ajili yetu hakika ni heshima kubwa kwa kanisa letu, "amesema baba Askofu Mkuu Shoo.
Wakati akihitimisha hotuba yake Mhe.Malima amegusia Swala la Mripuko wa Ugonjwa wa Ebola uliotokea Nchi ya Jirani ya Uganda na kusisitiza kuwa mbali na kuchukua tahadhari zote ni lazima Swala la kumshirikisha na kumuomba Mungu ni la msingi sana pia kuendelea kutoa Elimu maeneo ya ibada ili kuendelea kuchukua Tahadhari.
"Tunaomba muiunge mkono Serikali yenu na muiwezeshe kufanya kazi hiyo, tunaomba ushirikiano wakati wote na tunaomba muendelee kumuombea Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan na kuiombea Serikali kwa ujumla katika sala zenu za kila siku ili iweze kutuongoza kwa haki na kuwaletea Watanzania wote Maendeleo, kwa maana imeandikwa kwenye kitabu cha Mithali: 29.2 kuwa,Wenye haki wakiwa na amri,watu kufurahi, bali mwovu atawalapo,watu huugua, amesisitiza.
Naye Katibu Mkuu KKKT Mhandisi Robert Kitundu akimshukuru Mkuu wa Mkoa huyo amesema kuwa, anamshukuru sana kwa kuwatia moyo kwani kwa Mhe.Malima kufika na kusema maneno hayo wamejawa na Neema tele na kumuahidi kuwa yeye na wana KKKT wote watabaki wakimuombea.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.