Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Adam Malima amewakumbusha Makatibu Tawala Wasaidizi Mipango na Uratibu kutanguliza Weledi katika majukumu yao ili miradi ya maendeleo wanayoisimamia iwe na tija kwa Taifa.
Akifungua leo mafunzo ya siku tatu kwa viongozi hao kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa yenye lengo la kuwaelimisha namna ya kuandika na kusimamia miradi,Mhe Malima amesema viongozi hao ndiyo uti wa mgongo kwenye Ofisi za Mikoa kutokana na jukumu lao linalogusa maendeleo ya wananchi.
"Rai yangu kwenu zingatieni sana mafunzo haya huko mlikotoka natambua mna miradi mingi kuanzia Sekta ya afya na miundombinu,mkirudi muoneshe mageuzi chanya" amesema Mkuu huyo wa Mkoa.
Mhe Malima amebainisha Serikali ya awamu ya Sita imesambaza miradi mingi ikiwemo ya kimkakati kila kona ya nchi hii hivyo viongozi hao watambue mchango wao wa kuhakikisha ina ubora na kukamilika kwa wakati.
"Nami ni mchumi kama nyie hakuna nisichofahamu epukeni kutanguliza tamaa na kuhujumu miradi mnayosimamia na pia kuwa na kauli za kilaghai ili kuwafurahisha Viongozi wenu,mkifanya hivyo mtarudisha nyuma ndoto za wananchi za kupata maendeleo" amesisitiza Mhe.Malima
Awali akimkaribisha mgeni rasmi,Mkurugenzi msaidizi Idara ya Tawala za Mikoa kutoka TAMISEMI,Johnson Nyingi amesema mafunzo hayo yamewajumuisha Makatibu Tawala Wasaidizi kutoka Mikoa 25,wakiwezeshwa na Wataalamu wa masuala ya Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Mafunzo hayo yanafanyika Mwanza,.Mkoa ambao una Miradi mikubwa ya kimkakati yakiwemo Masoko,Stendi za mabasi,Reli ya Kisasa SGR, ujenzi wa Meli mpya ya Mv Mwanza pamoja na Daraja la JP Magufuli.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.