Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Adam Malima amewataka Halmashauri wanachama wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Kanda ya Ziwa Victoria, LVRLAC kusimamia na kuendeleza rasilimali za Ziwa Victoria ili ziendelee kuwa na tija kwa wananchi kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mhe. Malima akizungumza leo wakati wa kufungua mkutano mkuu wa 27 wa Taasisi hiyo Jijini Mwanza amesema Madiwani wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha wanaweka mikakati ya kisasa ukiwemo muda wa uvuaji wa samaki bila kuhofia nafasi zao za kisiasa kwa lengo la kuzidi kulifanya ziwa hilo kuwa nguzo muhimu ya uchumi.
"Ndugu zangu Madiwani nyie lazima matumbue mna changamoto kubwa ya kupaza sauti kwa niaba ya wananchi mnao wawakilisha,tukifanya mambo kwa kuingiza siasa hili Ziwa letu litageuka kuwa jangwa kwa maana ya kutoweka kwa rasilimali zilizomo ziwani humo".Amehimiza Mkuu huyo wa Mkoa.
Amesema Serikali sasa imetoa fedha nyingi kwenye Sekta ya Uvuvi na Kilimo waitumie fursa ya asilimia kumi inayotengwa na Halmashauri kuwawekea mazingira mazuri ya kujiajiri vikundi vya Vijana kwa kujikita kwenye kilimo cha umwagiliaji na ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba pamoja na Utalii.
"Ziwa letu lina visiwa vingi sana kama vile Ilugwa,Gana na Mbinguni huko kuna vivutio vingi ambavyo tukivitumia vizuri vitaleta watalii wengi na kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla"RC Malima.
Aidha ameshauri mikutano ijayo ya Taasisi hiyo wawajumuishe Taasisi za Kimataifa zinazojihusisha na masuala ya mazingira,Wakuu wa Mikoa,na Wakuu wa Wilaya ili agenda zao zibebe uzito na kufanyiwa kazi kikamilifu.
Akimkaribisha mgeni rasmi kufungua mkutano huo Mwenyekiti wa Taifa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Kanda ya Ziwa Victoria LVRLAC,William Gumbo amesema Taasisi hiyo yenye jumla ya Halmashauri 130 kutoka Tanzania na nchi wanachama Kenya na Uganda imeweza kupiga hatua katika majukumu yake ya kutunza mazingira ikiwemo kupanda miti na utunzaji wa ziwa Vitoria.
"Mhe mgeni rasmi miongoni mwa majukumu yetu kuyalinda mazingira ili yawe endevu kwa vizazi vijavyo pamoja na ziwa Victoria,nikiri bado tunahitaji nguvu ya pamoja katika kutimiza majukumu haya hasa upande wa ziwa bado zipo changamoto nyingi ikiwemo utumiaji usiyo sahihi wa ziwa Victoria kama kutupa taka ngumu,uvuaji haramu wa samaki yote haya yanahitaji uwajibikaji wa kweli ili kutimiza malengo tuliyoyakusudia."William Gumbo M/kiti LVRLAC Taifa.
Mkutano huo umejumuisha Halmashauri 47 kutoka Mikoa sita ya Geita,Shinyanga,Simiyu,Mwanza,Mara na Kagera huku Kauli mbiu yake ikisema Juhudi endelevu kati ya Tawala za Mitaa na Jamii katika kudhibiti mabadiliko ya Tabia nchi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.