Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Adam Malima amewataka wafatifi wa mazao ya Uvuvi nchini waje na matokeo yenye tija hasa masoko ya nje ya nchi ili yawanufaishe zaidi wananchi.
Akifungua kwa niaba yake kwenye Warsha wa Wadau ya kupokea na kupitisha taarifa ya Utafiti kuhusu upotevu wa Mazao ya Uvuvi nchini iliyofanyika Jijini Mwanza,Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Bw.Balandya Elikana amesema bado Uvuvi wa dagaa ambao ni wa kiwango kikubwa haujawa na tija ya kuinua kipato cha mwananchi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa soko la uhakika.
"Kwa mujibu wa Utafiti wa mwaka 2020 umeonesha Uvuvi wa kiwango cha dagaa ni asilimia 45 huku Sangara ni asilimia 33, lakini tujiulize unufaikaji tukianzia ubora wa bidhaa hadi kuuza unapitia kwenye hatua za kisasa? jibu ni hakuna hivyo bado tuna kila sababu ya kwenda na wakati ili kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla."Amehimiza Mtendaji huyo wa Mkoa.
Bw.Balandya ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Taasisi ya Utatifiti wa Uvuvi TAFIRI kwa kuonesha kujali na kutambua umuhimu wa Sekta ya Uvuvi nchini kwa kufanya Utafiti huo hasa mazao ya dagaa,hivyo ni matumaini kutapunguza changamoto au kuzimaliza kabisa.
Kaimu Mkurugenzi wa TAFIRI Hilary Mroso amesema ili kulinda usalama wa mazao ya uvuvi baharini na kwenye maziwa,utafiti kama huu utaendelea kufanyika ili kuhakikisha Taifa linakuwa salama kwa chakula na wananchi kwa ujumla.
"Ni jukumu letu kuimarisha mnyororo wa thamani kwa kusimamia njia zote bora na kisasa kwa mazao ya uvuvi hasa dagaa".Amesema Mroso.
Shirika la Kilimo na Chakula Duniani FAO limeziteua nchi tatu ikiwemo Tanzania,Sri Lanka na Colombia kutoka mabara matatu ya Afrika,Asia na Latin Amerika kuhusika na Utafiti wa upotevu wa mazao ya Uvuvi kwa lengo la kupata ufumbuzi,nini kifanyike na kuwepo mikakati endelevu ya usalama wa mazao hayo chini ya Udhamini wa Serikali ya Norway.
Utafiti huo umefanyika Bahari ya Hindi na kwenye maziwa Victoria na Nyasa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.