Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe Adam Malima amewataka wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya soka ya Dunia kwa wachezaji wanaotoka katika mazingira magumu itakayofanyika nchini Qatar mwezi huu kuzidi kuonesha uwezo na kurudi na Kombe la ubingwa.
Akizungumza na wachezaji hao kwenye ukumbi mkubwa wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa leo waliofika kumuaga,Mkuu huyo wa Mkoa amesema tangu michuano hiyo ianze mwaka 2010 huko Afrika Kusini, Tanzania imekuwa ikifanya vizuri kwa kushika nafasi za juu hivyo ana imani michuano ya mwaka huu watafanya vizuri.
"Nendeni mkashiriki hii michuano mkitanguliza mambo matatu,kwanza hii ni fursa yenu chezeni kwa uhodari mjulikane,pili wakilisheni vizuri Tanzania, tatu muwe na nidhamu ndani na nje ya michuano hiyo" amesisitiza Mhe Malima.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa amewakumbusha wachezaji hao mafanikio yao katika soka hayaji kwa miujiza bali ni bidii na kujitambua nini wanachotaka kufikia malengo.
Kocha mkuu wa timu hiyo Fulgence Novatus amebainisha Tanzania imeendelea kupata heshima ya kualikwa katika michuano hiyo kutokana na kuwa na rekodi nzuri kwani mwaka 2010 huko Afrika ya Kusini walifika hatua ya fainali kabla ya kutolewa na India,mwaka 2014 nchini Brazil walitwaa Ubingwa wa Dunia na mwaka 2018 iliyofanyika Urusi walishika nafasi ya pili kwa upande wa Wanawake.
Nahodha wa timu hiyo Warooba Warooba Kawambule amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa Mhe Malima Wana kila sababu ya kurudi na Ubingwa kutokana na uwezo walionao na maandalizi waliyopata.
Timu hiyo yenye jumla ya wachezaji 10 itaondoka kesho kuelekea Dodoma kukabidhiwa bendera ya Taifa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Mhe Dorothy Gwajima
Michuano hiyo inayochezwa kwenye Viwanja Maalum kwa kila timu kuwa na wachezaji 7 itaanza Septemba 11 hadi 15 mwaka huu ikishirikisha jumla ya Mataifa 28 kutoka Mabarara yote ulimwenguni.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.