Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima amewataka watekelezaji wa Mkataba wa Lishe Mkoani humo kutilia Mkazo Afua za Lishe ikiwa ni pamoja na kutenga fedha na suala hilo kuwa ajenda ya kudumu kwenye vikao ili kuondoa tatizo la Udumavu na utapiamlo kwa watoto.
Mhe. Malima amebainishwa hayo leo Septemba 21, 2022 wakati wa Mkutano wa tathmini ya Mkataba wa Lishe ulioangazia Afua za kufanikisha huku akibainisha kuwa Ukamilishaji wa miradi ya Maji kwa wakati na Mkazo wa Elimu kwa watoto kuwa ni miongoni nyenzo za kufanikisha lishe bora.
"Kila tunapokaa kwenye vikao vyetu tuweke ajenda ya lishe ili watu watambue nini kinaendelea na mambo yanayosababisha lishe duni ni pamoja na Matunzo duni ya mama na mtoto, tamaduni zisizofaa kama nyama kula baba pekee na ulaji usiofaa wa vyakula hivyo lazima tuepukane nayo na tuongeze uelewa wa umuhimu wa lishe kwa jamii." Amesema Malima.
"Mhe. Mkuu wa Mkoa, Viashiria vinaonesha tunakwenda vizuri kilichobaki ni wadau wote kuendelea kushirikiana katika kutekeleza shughuli za mkataba wa lishe ili kujenga pia jamii yenye afya njema." Amesema Katibu Tawala wa Mkoa, Balandya Elikana.
Mkuu wa Wilaya ya Magu, Mhe. Salum Kalli amesisitiza kuwa kwa kuzingatia Mkoa umekua ukifanya vizuri kwenye masuala mbalimbali kama Chanjo ya Uviko 19 ambapo Wilaya ya Ukerewe imekua Kinara, basi wataalamu wanapaswa kusimama imara kwenye kila kitu kama Ukusanyaji wa mapato ili uboreshaji wa Miundombinu ya Afya uende sambamba na uboreshaji wa afua za Lishe.
"Twendeni tukazingatie sana masuala haya ili tunapowasilisha taarifa za masuala ya Lishe kwenye ngazi ya Taifa Mkoa wa Mwanza kwa umuhimu wake tuwe wa kwanza kwenye utekelezaji wa Afua za lishe katika kuzingatia jamii inaimarika" Mhe. Kalli.
"Kwa mwaka huu kuna unafuu mkubwa kwenye kipengele cha fedha kwani Halmashauri zimepelekeka fedha kwa zaidi ya asilimia 70 ya fedha zinazohitajika kwenye afua za Lishe tofauti na asilimia 50 pekee ya fedha zilizopelekwa mwaka uliopita, lakini vilevile bado tuna changamoto ya upelekeji wa chakula chenye virutubisho kwenye shule." Amesema Dkt. Thomas Rutachunzibwa, Mganga Mkuu wa Mkoa.
Akichangia mada ya Magonjwa mlipuko, Mganga Mkuu ametoa wito kwa Halmashauri kuandaa maeneo ambayo yatapokea wagonjwa wa Ebola endapo watatokea na waisisitize jamii kuchukua tahadhari zinazotolewa na wataalamu wa Afya katika kujikinga dhidi ya ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa mara moja atakapotokea mgonjwa.
Naye, Mratibu Huduma za Chanjo Mkoa Amos Kiteleja amezitaadharisha Halmashauri kujiandaa na Mlipuko wa Ugonjwa wa Surua kwani kuna viashiria kutokana na kuwa na wagonjwa watano wa tatizo hilo na vilevile ameipongeza Halmashauri ya Buchosa kwa kufikia asilimia 90 ya utoaji chanjo za magonjwa mbalimbali na kufikia lengo la Taifa.
Awali Dkt. Mabai Leonard Mratibu Huduma za Matibabu ya Magonjwa ya Mlipuko Mkoa amesema kuwa katika kukabiliana na Mlipuko wa Ugonjwa wa Ebola wataalamu wameshaanza kutoa Elimu ya jinsi ya kujikinga na kwamba kimeshaandaliwa kituo maalum cha kutolea huduma hizo endapo atatokea.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.