Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Adam Malima amewakaribisha Wananchi wote na wale kutoka Mikoa jirani kuja Kwa wingi siku ya kesho kushuhudia Meli ya Mv Mwanza HAPA KAZI TU kutolewa kwenye chelezo na kuingizwa Ziwani Viktoria.
Akizungumza leo na Vyombo vya habari kwenye Ukumbi mkubwa wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa,Mhe.Malima amesema hii ni hatua ya pili kubwa katika ukamilishaji wa ujenzi wa Meli hiyo ambayo ni historia kwenye vyombo vya usafiri wa majini kwenye maziwa makuu hapa nchini.
"Tuna kila sababu ya kuishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye ameendelea kukuza Uchumi wa Taifa letu kwa vitendo hivyo Wananchi tuna kila sababu ya kuja kuyashuhudia matokeo chanya ya Miradi hii ya kimkakati".Amesema Mkuu wa Mkoa.
Mhe.Malima amebainisha baada ya chombo hicho kuingizwa majini, mwezi Juni mwaka huu litafuata tukio la Meli hiyo kuanza kutoa huduma.
"Hili ni tukio muhimu na la kihistoria kwenye nchi yetu na ukanda wa Afrika wenye Maziwa ambapo hii ndiyo Meli kubwa kuliko zote,uzito wa tano 3500, urefu wa mita 92.6, na Upanga wa mita 17, tujivunie mradi huu mkubwa"Eric Hamiss Mkurugenzi wa Kampuni ya Huduma za Meli.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Huduma za Meli Meja Jenerali mstaafu John Mbungo amesema hili ni tukio kubwa na kihistoria kwa nchi za Afrika Mashariki ni uwekezaji wenye tija ambao wananchi wana kila sababu ya kuishukuru Serikali ya Dkt.Samia.
Meli ya Mv Mwanza HAPA KAZI TU ilianza kujengwa Januari 2019 na Kampuni ya GAS Entec Limited kwa kushirikiana na Suma JKT kwa gharama ya Shs Bilioni 109.15.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.