Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima amesema yupo katika mkakati kamambe wa kupanda jumla ya miche ya miti milioni 3 Mkoani humo ili kukabiliana na tishio la ukame na kupungua kwa uoto wa asili.
Akizungumza leo na Viongozi na wanachama wa Shirikisho la Walimu Makada wa CCM kwenye Shule ya Sekondari Lugeye Wilayani Magu wakati akiongoza kampeni ya kupanda miche 400 ya miti, Mkuu huyo wa Mkoa amesema miti ina faida nyingi katika maisha ya Binadamu hivyo kuna umuhimu wa kuitunza.
"Katika maisha ya Binadamu hana mbadala wa chakula na maji ambapo chanzo chake ni uwepo na miti, hivyo vizazi vyetu na vijavyo ni lazima vielimishwe vya kutosha kuhusu umuhimu wa miti," amesema Mkuu wa Mkoa.
Mhe. Malima amebainisha kuwa Mataifa yaliyoendelea huwezi ukasikia wamekumbwa na ukame hii ni kutokana na kuelimika vyema tangu zamani kuhusiana na thamani ya miti na misitu kwa ujumla.
"Leo naongoza kupanda miche hii 400 lakini nawahakikishia nitakuwa nafuatilia maendeleo yake nikiwa na nia ya kutaka Sekondari hii ya Lugeye iwe ya mfano wa kuigwa kwa kuwa na utitiri wa miti" amesisitiza Mhe. Malima.
Awali akimkaribisha wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Magu Mhe, Salum Kalli amesema maagizo yote yaliyotolewa na Mhe Malima kazi yao ni kuyatekeleza hasa wakitambua umuhimu wa miti na mazingira bora kwa mwananchi.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Walimu Makada wa Chama cha Mapinduzi Mkoani Mwanza, Jackson Kadutu amesema katika kuiunga mkono Serikali ya awamu ya Sita wameamua kupanda miche hiyo pamoja na kugawa taulo za kike zenye thamani ya Shs milioni mbili na nusu kwa wanafunzi 300 na wengine 150 wenye mahitaji maalum.
"Huu ni utaratibu tuliojijengea kwa muda mrefu na mwaka huu tumefanya hivi pamoja na kukukaribisha rasmi Mkoani Mwanza Mkuu wetu wa Mkoa" amesema Kadutu.
Aidha Shirikisho hilo lenye mchanganyiko wa Walimu wa Vyuo, Sekondari na Msingi, limeshirikisha Halmashauri zote za Mwanza kwa kupanda miche 10,000.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.