Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima amepania kuinua zao la Pamba lenye ubora kwa kuweka shamba la mfano kata ya Buyagu Wilayani Sengerema.
Akizungumza na baadhi ya wakulima alipotembelea mashamba yao ya Pamba, Mhe. Malima amesema bado wakulima wa zao hilo hawatumii kilimo cha kisasa, sasa ameamua kuwasilisha mpango wa kuweka kilimo cha kisasa Bodi ya Taifa ya Pamba baada ya kupata hekari za kutosha kwa kuwatumia wakulima ambao watakuwa tayari kuingia katika mpango huo.
"Mimi ni Mwenyekiti wa kamati ndogo ya Uzalishaji wa zao la Pamba kwenye bodi ya Taifa, nitatumia fursa ya kikao chetu kijacho huko Mkoani Simiyu kuuzungumzia mpango huu lengo ni miaka michache ijayo mkulima avune tani milioni moja." Malima amesisitiza.
Amebainisha kuwa mpango huo utahusisha kuwaleta wakulima Wataalamu watakaopima udongo, kutoa ushauri aina ya mbolea husika na namna ya upandaji kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo ili mkulima kila hekari moja apate kilo 2000.
Ameongeza kuwa mara baada ya kuyakagua mashamba hayo amesikitishwa kutokana na kuwaona wakulima wakipoteza fursa ya kupata fedha nyingi kama wangetumia ulimaji wa kisasa unaohimizwa.
"Hapa nimelima kwa kutumia utaratibu wa kienyeji tu sijatumia utaalamu wowote wala kuweka mbolea, hii imetokana na kutofikiwa na Wataalamu nikaamua nilime tu nilivyozoea." Maneno Maneno, Mkulima wa Pamba.
Mkoa wa Mwanza unalima Pamba Wilaya 4 za Sengerema,Kwimba,Misungwi, na Magu na mwaka jana imevuna Pamba kilo milioni 16.
Aidha Mhe. Malima akiwa njiani kwenda Mgodi wa Nyanzaga kupata taarifa za maendeleo ya fidia za wakazi jirani na eneo hilo, amesimama kata ya Igarula katika mkutano wa hadhara na wananchi na kuwahakikishia mradi wa maji wa Shs Bilioni 13.7 unaotekelezwa na SEWASA kuwa utakamilika kwa wakati.
Kuhusu changamoto ya uchache wa Bweni Shule ya Sekondari ya Ngoma, Mhe.Malima ameahidi kuongeza mabweni mawili la wasichana na wavulana ili kuwapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu wanafunzi hao.
"Niwasihi sana wananchi muwe na utulivu na msikubali kudanganywa na wachache watakaokuja kwa nia ya kuchochea migogoro wakati mkiwa mbioni kulipwa fidia na Mgodi wa Nyanzaga". Amesisitiza Mkuu huyo wa Mkoa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.