Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella amewataka Wakurugenzi watendaji wa Jiji la Mwanza, Kwimba na Buchosa kuchukua maamuzi ya mapendekezo yaliyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa(NECTA) na Naibu Katibu Mkuu wa Elimu Tamisemi waliyoyatoa wakati wanatangaza kufuta matokeo ya darasa la saba kwa shule zilizohusika na wizi wa mitihani zikiwemo tatu za jiji la Mwanza.
Mhe. Mongella amesema wamiliki wa shule, wakuu wa shule na baadhi ya walimu ndiyo wahusika wakuu wa kuiba mitihani wakiwa na lengo la kufaurisha watoto wengi ili wazazi waamini shule husika na kupeleka watoto wengi zaidi katika shule hizo.
“Ninawasiwasi hata kwenye idara zetu za elimu kuna watu wanahusika, ninachokitegemea wote walioelekezwa kuondolewa kwenye nafasi zao wakisubiri mamlaka zao kufanya maamuzi kufikia leo saa sita ,maamuzi yawe yamechukuliwa sitegemei mkurugenzi wa kwimba, jiji la mwanza na Buchosa kutofanya maamuzi, tutamfanyia yeye maamuzi,”alisema Mongella.
Aliwataka wamiliki na wakuu wa shule wenye tabia ya kuiba mitihani waache kwa kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kuvuliwa wadhifa wao na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dkt.Philis Nyimbi alisema waliokamatwa kwa kuiba mitihani inaonekana walianza muda mrefu kwa kuwa za mwizi ni 40 ndio maana wamekamatwa.
“Tumesikitishwa sana Wilaya yetu kutiwa doa la wizi wa mitihani na baadhi ya watu wachache wasio waadilifu licha ya wilaya kujitahidi kufanya mambo ya kuleta maendeleo,”alisema Dkt. Nyimbi.
Hata hivyo Mhe.Mongella amewaagiza Takukuru na polisi kuchukua hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kukamatwa wakati wakisubiri Mamlaka zao kufanya maamuzi.
"Kufikia leo saa sita kama kuna mtu amefanya uzembe wa kutochukua maamuzi,atafanyiwa yeye maamuzi, nawahitaji walioguswa na hilo, REO nataka nione barua zote za maamuzi hayo,"alisema Mhe. Mongella.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.