Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongella ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA) kwa kubuni na kuendeleza Mfumo wa kupima utendaji wa watumishi wake kikanda ambao alisema unaleta ufanisi wenye tija.
Pongezi hizo alizitoa Oktoba 01, 2018 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Mamlaka hiyo katika hafla ya kukabidhi zawadi kwa watumishi wa Kanda ya Makongoro ambayo ilishinda vigezo vinavyotumika kupima utendaji wa watumishi kikanda ambavyo ni mauzo na makusanyo.
Mfumo huo wa upimaji wa utendaji kwa watumishi wa MWAUWASA ulizinduliwa rasmi Agosti, 2018 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo ambao unapima utendaji wa watumishi kikanda kupitia kanda zake mbazo ni Makongoro, Nyegezi, Nyakato na Kanda ya Mjini Kati.
Katika mashindano hayo kwa mwezi Septemba, Kanda iliyoongoza ni Makongoro kwa kupata asilimia 96.35 ikifuatiwa na Kanda ya Mjini Kati asilimia 96.07, Kanda ya Nyegezi asilimia 95.36 na mwisho ni Kanda ya Nyakato asilimia 94.99.
Akizungumzia mfumo huo, Mhe. Mongella alisema upimaji wa utendaji kwa kushindana unapaswa kuigwa na wengine ili kuleta matokeo chanya kwenye shughuli mbalimbali hasa ikizingatiwa kwamba wananchi wanahitaji huduma bora kwa ajili ya kujiletea maendeleo.
"Pongezi kwenu Bodi, Menejimenti na Watumishi wa MWAUWASA kwa kubuni huu mfumo wa kushindana ambao na wengine wanapaswa kuiga ili kupiga hatua,” alisema Mongella.
Alizipongeza Kanda zote Nne kwa jitihada walizoonyesha kuhakikisha wanatimiza malengo waliyojiwekea. “Ukiona mtu anajiwekea malengo na anapambana kufikia malengo huyo anaweza,” aliongeza Mhe. Mongella.
Mongella alisema kwa namna ambavyo Mamlaka hiyo inavyoendesha shughuli zake ni dhahiri kwamba itaendelea kuwa kinara miongoni mwa Mamlaka za Maji nchini kwa utendaji bora.
Hata hivyo, Mongella aliwataka wafanyakazi wa Mamlaka hiyo kuwa wabunifu zaidi ili kwenda mbali zaidi katika utoaji wa huduma sambamba na kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji kwenye maeneo mbalimbali ya Jiji na viunga vyake.
Alisema wananchi wanahitaji upatikanaji wa huduma bora ya maji kwa maendeleo endelevu na kwamba ni jukumu la kila mtumishi wa Mamlaka hiyo kuhakikisha hayo yanafikiwa.
Aliwataka watumishi kutoka Kanda ya Makongoro kuhakikisha wanabakia kwenye nafasi hiyo kwa kutobweteka badala yake kuongeza ubunifu, maarifa na juhudi zaidi kwenye utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
"Watumishi wote wa MWAUWASA fikirieni namna ya kuongeza upatikanaji wa maji maeneo mengi sambamba na kuboresha upatikanaji wa mapato; na haya ndio mafanikio,” alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya MWAUWASA, Christopher Gachuma alipongeza umoja na mshikamano miongoni mwa watumishi na aliwataka waendeleze hayo kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.
Gachuma alisema mafanikio yanayoonyeshwa na Mamlaka hiyo ni uongozi thabiti na mahiri wa Mkurugenzi Mtendaji wake sambamba na mshikamano uliyopo miongoni mwa watendaji na aliwaasa kuhakikisha wanauendeleza na kuuzidisha kila inapobidi.
Akizungumzia vigezo vilivyotumika kupata mshindi wa kanda iliyofanya vizuri kwa Mwezi Septemba, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo, Mhandisi Anthony Sanga alivitaja kuwa ni mauzo na makusanyo.
Hata hivyo alisema vigezo vitaongezwa kutoka viwili hadi vitano ambavyo kwa ujumla wake alivitaja kuwa ni mauzo, makusanyo, maunganisho mapya ya wateja, uharaka wa kutatua malalamiko ya wateja hususan suala zima la upatikanaji wa maji, udhibiti wa upotevu wa maji kwa kiwango kinachokubalika.
Mhandisi Sanga alibainisha kwamba lengo kubwa la mfumo huo ni kuongeza makusanyo, kuongeza mauzo ya maji lakini pia kuhakikisha maji yanafika kila kona ya jiji la Mwanza na viunga vyake kwa maana ya usambazaji wa maji, kupunguza upotevu wa maji sambamba na kuhakikisha wateja wote wanaunganishwa kwenye mfumo wa maji.
"Lengo ni kufika kwenye maeneo ambayo bado hatujayafikia ambayo tutayapelekea huduma kwa siku zijazo, hasa baada ya Mradi wa Uboreshaji wa huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira wa Ziwa Victoria (LV WATSAN) kukamilika” aliongeza Mhandisi Sanga.
Kuhusu zawadi ya Kanda iliyoshinda, Mhandisi Sanga alisema mbali na kupewa kombe, watumishi 24 kutoka kwenye Kanda husika watafanya ziara ya mafunzo kwenye Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Jijini Dar es Salaam (DAWASA) na Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) ili kuongeza uelewa wa masuala mbalimbali ya kiutendaji sambamba na kubadilishana uzoefu wa namna ya kutatua changamoto mbalimbali katika Sekta ya Maji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.