Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.John Mongella ametekeleza agizo lililotolewa na Mhe. Rais Dkt.John Pombe Magufuli juu ya kuhakikisha anasimamia na kuyafanyia maamuzi malalamiko ya wafanyabiashara wadogo Maarufu Machinga wilayani Sengerema.
Hii ni kufuatia maagizo ya Mhe.Rais Dkt.John Magufuli baada ya kupita Wilaya ya Sengerema akielekea Wilaya ya Chato kwa ajili ya mapumuziko na kusimama kwa ajili ya kuwasalimia, ndipo walipotoa malalamiko kuwa mnamo tarehe 10.8.2018 ilifanyika operation ya kuwaondoa wafanyabiashara ndogondogo, hiyo ilipelekea wafanyabiashara wa nanasi 11 wanaofanya biashara ya kuuza nanasi kandokando ya barabara kuchukuliwa na Halmashauri katika oparesheni hiyo.
Mhe.Mkuu wa Mkoa amemtaka mkurugenzi kulifanyia marekebisho soko lililipo karibu na eneo wanalouzia nanasi kwa sasa kwa kujenga mabanda ya nguzo za mabomba yatakayoezekwa kwa mabati ili kuwatengenezea kivuli baada ya hapo wafanyabiashara hao washirikishwe katika kupanga na kuhamia katika eneo hilo.
"Ifikapo jumatatu tarehe 20/08/2018 wale watu 11 waliochukuliwa biashara zao za nanasi waitwe na wafidiwe fedha kwa nanasi zao kuchukuliwa kwa jinsi watakavyokuwa wamekubaliana na ifikapo jumatano tarehe 22/08/2018 wawe wamelipwa fidia yao,"alisema Mongella.
Aidha Mhe Mongella amemuagiza mkurugenzi huyo kuwa maafisa maendeleo ya jamii watumike kwenda kwenye jamii kuwaelewesha na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa masuala mbalimbali yenye tija kwa kjamii na sio watu wa mapato ambao kazi yao ni kukusanya mapato.
Naye Jacob Mlinga mmoja kati ya wananachi walioathirika na kuchukuliwa nanasi zao na watendaji wa Halmashauri ya Sengerema amemwambia Mhe. Mkuu wa Mkoa kuwa alichukuliwa nanasi 700 yaliyokuwa kwenye matoroli mawili, ambapo baada ya kumsikiliza aliwaelekeza yeye na wenzake kwenda ofisini kwa mkurugenzi ambapo tatizo lao litashughulikiwa.
Kwa upande wake mfanyabiashara mwingine Elina Taibu anayejishughukisha na biashara ya umachinga amemshukuru Mhe.Rais John Pombe Magufuri kwa kuwajali wanyonge na ameomba aendelee kuwatetea na kushughulikia matatizo ya watu wa chini.
Hata hivyo Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Magesa Mafuru Boniface amewataka wafanyabishara waendelee kutoa ushirikiano kuhamia katika eneo lililotengwa la kisima cha chumvi, pia amempongeza Mhe. Rais kwa kusikiliza kero za wananchi wa Sengerema na kuahidi kutekeleza maagizo yote aliyoagizwa kuyatekeleza katika kushughulikia tatizo la wafanyabiashara
hao.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.