Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella amewataka viongozi wa Serikali mkoani Mwanza kuiga mfano wa Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mhe. Juma Sweda wa kuhakikisha wanawadhibiti watu wanaowapa ujauzito wanafunzi wa kike na hivyo kukatisha ndoto za maisha kwa kushindwa kuhitimu elimu yao.
Alimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mhe. Juma Sweda na Kamati yake ya ulinzi na usalama kwa hatua ambazo wamechukua za kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watu waliobainika kuwapa ujauzito watoto wa kike, akiwemo Mwalimu Peter Fred wa Shule ya Msingi Kifune wilayani humo ambaye amehukumiwa kifungo cha miaka 30 kwenda jela baada ya kubainika kuwa na hatia ya kumpatia ujauzito mwanafunzi.
“Nilipomuona Mwalimu yule kupitia kwenye mitandao na Televisheni akiwa amepigwa pingu nilifurahi sana, ningekuwa na fedha ningemtumia DC wa Misungwi kwa kweli amefanya kazi kubwa sana," alisema Mhe. Mongella na kuwataka wakuu wengine wa wilaya kuiga mambo mazuri yanayofanywa na uongozi wa wilaya ya Misungwi katika kudhibiti mimba mashuleni.
Aidha aliwataka wakuu wa wilaya za Ukerewe na Kwimba kuhakikisha wanadhibiti mimba mashuleni, pamoja na wilaya nyingine ili kuboresha elimu kwa mtoto wa kike.
“Kwimba hali ya utiaji wa mimba inatisha, utafikiri wilaya ina mpango maalum wa utiaji mimba kwa wanafunzi na DC mwanamke upo," alisema Mhe. Mongella.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Magu Mhe. Dkt. Philemoni Sengati alikiri kulishughulikia suala la mimba katika wilaya yake, lakini juhudi hizo zimekuwa zinakwamishwa na baadhi ya watendaji wa mahakama kushindwa kutoa haki kwa watuhumiwa wanaokuwa wamebainika kuwapatia ujauzito watoto wa kike.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.