Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda, ameagiza kuchukuliwa hatua za haraka za kinidhamu na kisheria dhidi ya mtumishi wa umma aliyedaiwa kujihusisha na mgongano wa maslahi, wizi wa mali za Serikali na ucheleweshaji wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Mkoa yenye hadhi ya Rufaa unaotekelezwa Wilaya ya Ukerewe.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mradi huo, Mhe. Mtanda amesema changamoto ilianza pale ambapo kampuni ya Nosa, inayomilikiwa na mtumishi wa Serikali, ilipewa tenda ya kusambaza kokoto kwa ajili ya mradi huo, bila mhusika kutangaza maslahi yake (declare interest), jambo ambalo ni kinyume na sheria na maadili ya utumishi wa umma.

Mhe. Mtanda amesema mtumishi huyo alilipwa fedha za Serikali kupitia akaunti yake binafsi, lakini ameshindwa kusambaza kokoto kwa wakati, hali iliyosababisha ucheleweshaji wa mradi na kumkwamisha mkandarasi.

“Haya hatuwezi kuyakubali. Mtumishi wa Serikali kujipa tenda, asitangaze maslahi, alipwe kwenye akaunti binafsi halafu achelewesha mradi wa wananchi hili ni kosa kubwa,” amesema Mhe. Mtanda.

Ameeleza pia kuwa nondo zenye thamani ya shilingi milioni 9 ziliibwa na kuuzwa kwa shilingi milioni 2 kwa mtumishi huyo, huku aliyefanikisha uuzaji huo akiwa ni mtumishi wa Halmashauri. Amelipongeza Jeshi la Polisi kwa hatua ya kuwakamata watuhumiwa wa tukio hilo.

Kutokana na hilo, Mkuu wa Mkoa amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza (RAS) kuhakikisha mtumishi huyo anachukuliwa hatua za kinidhamu mara moja, huku Jeshi la Polisi (NPS) likitakiwa kufungua kesi ya jinai na kumfikisha mtuhumiwa mahakamani Mwanza.

“Huyu mtumishi hatakiwi kulindwa hapa Ukerewe. Hii ni kesi ya wizi. NPS andikeni kesi inayomfaa na ahukumiwe kwa mujibu wa sheria. Tusipofanya hivyo, mradi huu utachelewa kukamilika,” amesisitiza.

Mhe. Mtanda amesema kucheleweshwa kwa mradi huo kutawafanya wananchi kuichukia Serikali, licha ya Serikali Kuu kutoa zaidi ya shilingi bilioni 26 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo, akionya kuwa watu wachache hawapaswi kuhujumu juhudi za Serikali za kuboresha huduma za afya.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.