RC MTANDA AAGIZA VITUO VYOTE VYA AFYA MWANZA KUFUNGWA MFUMO WA GoTHOMIS HARAKA IWEZEKANAVYO
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka Wataalamu wa afya kusimika na kutumia ipasavyo mfumo wa kielektroniki wa kudhibiti ba kufuatilia taarifa za mteja (GoTHOMIS) ili kuongeza ukusanyanji mapato na utunzaji taarifa za wagonjwa.
Mhe. Mtanda Ametoa agizo hilo mapema leo Januari 09, 2025 wakati akifungua kikao cha mafunzo ya mifumo wa usimamizi wa uendeshaji Sekta ya Afya (GoTHOMIS) ambao unalengo kutunza kumbukumbu na kukusanya mapato kupitia uchangiaji wa huduma kwa jamii.
Amesema katika kutekeleza vema adhma ya mfumo huo ni lazima Wakurugenzi na Maafisa TEHAMA wa Halmashauri kukomesha utoaji wa huduma nje ya mfumo huo mara moja kwa huduma yoyote inayotolewa na kuhakikisha katika kila kituo kinafungwa mfumo huo.
"Mkoa unapimwa kwa usimamizi mzuri wa sera na maagizo ya kisheria, kanuni na afua mbalimbali yanayotolewa na Serikali na siyo vinginevyo, nami sitakubali kuwa wa mwisho kwenye usimamizi wa mfumo huu wa kukusanya mapato na nawataka mkasimamie vizuri." Mkuu wa Mkoa
.
Aidha, amewaagiza kila mmoja kusimamia majukumu yake vema ili kuhakikisha lengo linafikiwa na kwa ambaye atashindwa kufanya hivyo atamchukulia hatua za kinidhamu kwani hatokubali wakati wa tathmini ikionesha mkoa umeshuka.
"Twendeni tukakusanye mapato kupitia mfumo huu maana Serikali imeshasimika miundombinu tena kwa gharama kubwa, mfano katika Mkoa wa Mwanza kwa kipindi kifupi cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan tumeshapokea zaidi ya Tshs. Bilioni 49 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu." Amesisitiza Mkuu wa Mkoa.
Ameongeza kuwa mfumo huo una faida kadhaa ikiwa ni pamoja na mawasiliano baina ya kituo na kituo yaani mgonjwa ataonekana ameshahudumiwa wapi na anahitaji kuongezewa nini bila gharama na pia utunzaji wa taarifa kwa ufanisi.
Halikadhalika, ametoa wito kwa Wataalamu hao kwenda kusimamia suala la mfumo wa iCHF liwe ajenda kwenye vikao na mikutano ya hadhara inayoendeshwa katika ngazi za vitongoji, Vijiji/Mitaa na kata ili wananchi waelimishwe kufahamu faida za kuwa na bima hiyo.
Akitoa taarifa ya awali, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Jesca Lebba amebainisha kuwa Mkoani humo kati ya vituo 354 vinavyopaswa kufungwa mifumo hiyo ni 178 pekee ndio vimefungwa sawa na asilimia 56.2 na hata walikofunga matumizi ni ya kiwango cha chini na akawataka Waganga Wakuu wa Wilaya kuchapa kazi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.