RC MTANDA AAHIDI KUTATUA KERO ZA WAUGUZI MWANZA, AWAHIMIZA KUTOA HUDUMA BORA KWA WATEJA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ameungana na Wauguzi na Wakunga mkoani humo katika Kumbukizi ya mwanzilishi wa taaluma ya uuguzi Duniani, Florence Nightngale kwa kuwaahidi kutatua baadhi ya kero zao zikiwemo posho za sare za kazi na kupandishwa madaraja
Akizungumza na kada hiyo kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou Toure Mtanda amesema Serikali inatambua umuhimu na mchango wa wauguzi hivyo Ofisi yake itayafanyia kazi changamoto hizo.
"Mganga Mkuu wa Mkoa na wasaidizi wako nileteeni orodha ya watumishi wanaostahili kupandishwa vyeo nitakaa na Katibu Tawala kulifanyia kazi na pamoja na hiyo posho ya sare 120,000 kwa mwaka.
Mkuu huyo wa Mkoa amewakumbusha kuendelea kufanya kazi kwa weledi wakizingatia viapo vyao huku Serikali ikiendelea kuboresha mazingira yao ya kazi.
"Nimesikia katika risala yenu kuhusu upungufu wa watumishi kwa asilimia 40 hilo lipo kwa Serikali kuu na naamini litaendelea kufanyiwa kazi na Mamlaka husika"Mhe.Mtanda
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Thomas Rutachunzibwa amesema kwenye sekta ya afya bila wauguzi ni sawa na bure na siku zote wanaofanya kazi kwa zaidi ya uwezo wao,hivyo ni vyema wakapewa kipaumbele katika utatuzi wa changamoto zao ili kuwajengea ari ya kazi.
Kwa upande wake Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bi.Claudia Kaluli amesema licha ya uchache wao ambapo hadi sasa Mkoa una asilimia 60 ya wauguzi,wanaendelea kufanya kazi katika mazingira hayo wakiwa na matumaini ya hali hiyo kupatiwa ufumbuzi na Serikali.
"Ndugu mgeni rasmi siku hii hufanyika kila mwaka na sisi hapa Mwanza kuanzia Mei 29,2024 hadi leo tumefanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo upimaji wa Saratani ya shingo ya kizazi,magonjwa yasiyoambukiza pamoja na upimaji wa VVU na kutoa ushauri kwa wateja waliobainika na magonjwa husika na kuwapa ushauri wa kitabibu",Lucia Setembo,M/kiti wa chama cha wauguzi tawi la Seko Toure.
Siku ya Kumbukizi ya mwanzilishi wa taaluma ya uuguzi Duniani,Florence Nightngale imefanyika Kitaifa Mei 12,2024 .mkoani Tanga.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.