RC MTANDA AAHIDI USIMAMIZI MZURI WA KODI, ELIMU NA KUTAKA MALEZI BORA KWA VIJANA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo Aprili 11, 2024 ameshiriki Baraza la Eid El Fetr kama mgeni rasmi na kuahidi usimamizi mzuri wa Kodi bila kuonewa mtu, asisitiza elimu na amewataka wazazi kukumbuka wajibu wao wa malezi bora vijana.
Akizungumza na washiriki wa Baraza hilo kwenye ukumbi wa BoT, Mkuu huyo wa Mkoa amesema hakuna Taifa lolote lililoendelea bila ya kuwa na mpango mzuri wa ulipaji wa kodi hivyo atasimamia kikamilifu na kutanguliza uungwana kwa wafanyabiashara.
"Sipo tayari kuona nguvu ikitumika katika utekelezaji wa sheria za nchi iwe kwa mwananchi yoyote wakiwemo wafanyabiashara, napenda mashauriano zaidi na kuchukua maamuzi," amesema Mtanda.
Kuhusu suala la elimu amesema ni wajibu wa kila mzazi kutimiza haki za watoto wao kwa kuhakikisha wanakwenda shule kikamilifu.
Akizungumza suala la malezi Mtanda amekemea tabia iliyoibuka hivi sasa kwa baadhi ya Wanawake wenye vipato kujigamba wao ni 'SINGLE MOTHER' na kusisitiza malezi bora ni kwa wazazi wote wawili
"Familia yenye malezi bora kwa watoto wao mnaturahisishia hata sisi viongozi kuwaongoza watu wenye weledi wa tabia hivyo Taifa linakuwa na watu waliostaarabika.
Aidha amewakumbusha viongozi wote wa dini kuendelea kuwaombea viongozi wetu wa juu kuwa na afya njema na hekima ya kuliongoza Taifa letu.
"Rais Samia katuletea miradi mingi ya kimkakati yenye thamani ya ma trioni ya fedha ikiwemo reli ya kisasa SGR,Meli ya Mv Mwanza,Daraja la JP Magufuli na sasa unapanuliwa uwanja wa ndege uwe wa knimataifa,ni wajibu wa kila mmoja kumshukuru na kumuombea",RC Mtanda.
Akimkaribisha mgeni rasmi kwenye Baraza la Eid,Shehe mkuu wa mkoa wa Mwanza,Hassan Kabeke amesema wao kama viongozi wa dini wataendelea kuiunga mkono Serikali katika ujenzi wa Taifa na tayari wana kauli mbiu kwa waumini wao isemayo Shiriki uchaguzi mdogo wa Serikali za mitaa kwa utulivu na amani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.