RC MTANDA AFUNGA MAFUNZO YA UFUGAJI SAMAKI, AHIMIZA KUCHANGAMKIA FURSA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo Machi 28, 2025 amefunga mafunzo ya ufugaji wa samaki kwa njia ya Vizimba na kutoa rai kwa vijana kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali.
Akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo ya siku 15 kwenye chuo cha wakala wa Elimu ya Uvuvi Feta, Nyagezi wilayani Nyamagana, Mkuu huyo wa Mkoa amebainisha kuwa hakuna sababu za vijana kukaa vijiweni wakati zipo fursa mbalimbali za kuwainua kiuchumi.
Amesema Serikali ya awamu ya sita kwa kutambua nguvu kazi ya vijana imetoa fedha nyingi katika mradi wa ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ambao umekuwa na tija katika awamu hii ya kwanza.
"Jumla ya boti 160 za kisasa za uvuvi zimetolewa kwa wanufaika 3, 295 na vizimba 222 kwa wanufaika 1,214 na mikopo hiyo imetolewa bila riba na benki ya maendeleo ya kilimo Tanzania TADB", Mhe. Mtanda
Aidha amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuja na mageuzi chanya baada ya kupata mafunzo hayo hasa kuongeza Uzalishaji wa samaki ambao takwimu zinaonesha bado upo chini kutokana na sababu mbalimbali ukiwemo uvuvi haramu na tabia nchi.
Mhe.Mtanda ameipongeza pia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuandaa mafunzo hayo yenye lengo la ukuzaji viumbe maji na pia kukuza biashara kupitia rasilimali hizo.
Ameongeza kuwa bado ulaji wa samaki kwa mtanzania kwa mwaka upo chini ambao ni kilo 7-8 wakati inatakiwa ulaji uwe kilo 20,hivyo mafunzo hayo yatakuwa ni muarobaini wa changamoto hiyo.
Kwa upande wake Meneja wa Kampasi ya Mwanza kutoka chuo cha wakala wa Elimu ya Uvuvi FETA Bw.Steven Lukanga amesema kwa siku 15 washiriki hao wamejifunza ukuzaji wa samaki kibiashara na masoko yake,kuhakiki ubora wa maji,afya na magonjwa ya samaki,mfumo wa ukuzaji wa samaki na utengenezaji wa vyakula na Uzalishaji samaki kwenye vizimba.
"Tunaishukuru Serikali kwa kuendelea kuiinua na kuiboresha sekta ya Uvuvi hapa nchini,ombi letu kama chuo itambuliwe mipaka kati ya wavuvi wa asili na wenye vizimba kutokana na kuibuka kwa migogoro ya mara kwa mara",Makanga.
Jumla ya washiriki 172 ambao ni wafugaji samaki na Maafisa Uvuvi kutoka mikoa ya kanda ya ziwa pamoja na Dar-e-s-Salaam,Lindi,Morogoro na Pwani wamepata mafunzo hayo na kutunukiwa vyeti.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.