RC MTANDA AFUNGA RASMI MICHEZO YA SHIMISHEMITA MWANZA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda akimuwakilisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) leo Septemba 5, 2024 amefunga rasmi Michezo ya Shirikisho la Michezo ya Serikali za Mitaa (SHIMISEMITA) kwenye uwanja wa Nyamagana Jijini Mwanza.
Akizungumza na wanamichezo hao Mhe. Mtanda amesema Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuinua sekta ya michezo, sanaa na utamaduni na ni muhimu kwa watumishi wa Serikali kumuunga mkono mchezaji namba moja nchini ambaye ni Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kushiriki katika michezo hiyo iliyoandaliwa kwa ajili yao.
"Michezo mahala pa kazi inawajengea ari ya kuchapa kazi kwani ukamilifu wa afya inawajengea uwezo mkubwa wa kufanya kazi tena kwa weledi, huku mkiwaa mmeimarika wakati wote lakini pia ina wajengea uzalendo." RC Mtanda.
Aidha, amewataka wanamichezo hao kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za michezo ili malengo ya shirikisho hilo yatimie na ametumia jukwaa hilo kuzionya Halmashauri zilizokiuka taratibu na kupelekea kuondolewa kwenye michezo hiyo kuhakikisha hawafanyi hivyo tena kwani kuwapelekea watumishi kuwakosesha haki yao ya kujumuika na wenzao katika michezo.
Sambamba na hayo Mhe. Mtanda piaa amewapongeza wanamichezo kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela na Wilaya ya Kwimba kwa Mkoa wa Mwanza kwa kushika nafasi za tatu kwenye baadhi ya michezo.
Awali, Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo Henry Kapela alibainisha kuwa jumla ya wanamichezo 2160 kutoka kwenye Halmashauri 100 wameshiriki mwaka huu tofauti na 45 za mwaka jana na kwamba uhamasishaji na maandalizi ya michezo ya mwakani unapaswa kuanza sasa.
Vilevile, ametoa rai kwa uongozi wa mashirikisho hayo ngazi ya Halmashauri kuzingatia taratibu na sheria za michezo chini ya shirikisho hilo ili kuwaepusha na usumbufu wa kuondolewa kama ilivyotokea kwa halmashauri 3 ambazo ni Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Dodoma na Manispaa ya Moshi.
Mshindi wa jumla wa michezo ya SHIMISEMITA kwa mwaka huu ni Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambao wamekua wa kwanza kwa michezo 9. Aidha michezo hiyo kwa mwaka huu imechagizwa na kaulimbiu isemayo "Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Taifa Endelevu".
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.