RC MTANDA AHIMIZA UTEKELEZAJI WA MFUMO WA GoTHOMIS NA LISHE
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Said Mtanda amefungua kikao cha kamati ya afya ya msingi mkoani humo na kuhimiza utekelezaji wa mfumo wa taarifa za usimamizi wa uendeshaji wa afya wa Serikali ya Tanzania katika vituo vya huduma za afya(GoTHOMIS) na afua za Lishe lengo likiwa Mkoa huo uwe kinara Kitaifa katika utoaji bora wa huduma hizo.
Akizungumza na wajumbe wa kamati hiyo leo Machi 12, 2025 kwenye ukumbi wa Ofisi ya mkuu wa mkoa, Mtanda ametoa maelekezo kwa Mganga Mkuu wa Mkoa kuhakikisha mfumo huo unafungwa kwenye vituo vyote vya afya na apatiwe taarifa ya maendeleo yake kabla na baada ya matumizi hayo.
Amesema kwa mujibu wa takwimu Mkoa wa Mwanza unashika nafasi ya 3 kitaifa kwa utekelezaji wa huduma ya GoTHOMIS, amehimiza kazi ya ziada iendelee kufanyika ili tushike nafasi ya kwanza.
"Serikali inaendelea kuwekeza katika miradi ya afya, lakini hatuna budi kuhakikisha yanakuwepo makusanyo sahihi ya fedha ili zisaidie kuboresha huduma hiyo na nyinginezo", Mkuu wa Mkoa.
Kuhusu afua za Lishe, Mkuu huyo wa Mkoa amewakumbusha maafisa lishe kutoka halmashauri zote mkoani humo kuhakikisha wanafanya vizuri ili kuepukana na hali ya udumavu na ukosefu wa afya kwa watoto walio chini ya miaka mitano.
"Hapa Afisa Lishe Mkoa ametupitisha katika taarifa yake bado Halmashauri nyingi hazifanyi vizuri,na hili ni agizo la Mhe.Rais kwa sisi wakuu wa mikoa kulisimamia vizuri zoezi hili,sasa sitakuwa tayari kuona baadhi ya maafisa lishe mkifanya uzembe,"amesisitiza Mtanda wakati akifunga kikao hicho.
Wakati huo huo, Waziri wa Afya Mhe. Jenister Mhagama amepata wasaa wa kuwasalimu wajumbe wa kikao hicho alipofika Ofisi ya mkuu wa mkoa akielekea katika majukumu mengine na kusisitiza bado magonjwa yasiyoambukiza ni changamoto na kutoa rai kubadili mtindo wa maisha ukiwemo ulaji na kufanya mazoezi.
Kikao cha kamati ya afya ya msingi ya Mkoa kimewajumuisha wakuu wa wilaya,wakurugenzi wa Halmashauri, waganga wakuu wa wilaya,maafisa lishe pamoja na viongozi wa dini.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.