RC MTANDA AKARIBISHA FURSA ZA UWEKEZAJI KATIKA MICHEZO
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mh.Said Mtanda leo Septemba 6,2024 amekutana na wataalamu wa michezo kutoka nchini Brazil na katika mazungumzo nao amewaalika kuwekeza katika michezo hasa kutokana na Mkoa huo kuwa na hazina ya vipaji.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ofisi kwake na wataalamu hao wa soka,Mtanda amebainisha licha ya kuwa na vijana wenye vipaji lakini tunakwama namna ya kuviendeleza hivyo bado tunahitaji nchi kama Brazil iliyopiga hatua kubwa katika sekta hiyo.
Mkuu huyo wa Mkoa ambaye ni mkereketwa wa mchezo wa soka amewaambia wataalamu hao kuwa watanzania wana imani kubwa na Taifa la Brazil katika mchezo wa soka hasa kutokana na hatua kubwa waliyopiga na vipaji walivyonavyo
Ameongeza kuwa michezo kwa sasa ulimwenguni ndiyo nguzo imara ya ajira, lakini kabla ya mchezaji huyo kupata soko ni lazima apitie misingi muhimu ambayo hapa kwetu bado wanaikosa.
"Ili mchezaji uwe wa Kimataifa ni lazima uwe na nidhamu,upitie timu za Taifa za vijana,na misingi mingine madhubuti kutoka shule maalum za michezo," amefafanua Mtanda wakati akitoa taarifa fupi kwa vyombo vya habari mara baada ya mazungumzo na wageni wake.
Kiongozi wa msafara huo ambaye pia amemwakilisha Balozi wa Tanzania nchini Brazil,Beatus Kalumuna amesema lengo la ziara hiyo kwanza ni kuimarisha uhusiano wa Diplomasia ya michezo baina ya Tanzania na Brazil na kubadilishana uzoefu wa kitaalamu pia kupitia sekta hiyo.
"Hapa wamekuja wataalamu tofauti wakiwemo wa kuibua vipaji,wa kuviendeleza,mwakilishi kutoka Cruzelo shule ya soka ya mchezaji Ronaldo Nazari de Lima na mtaalamu wa michezo ya Olympiki,"Kalumuna
Wakiwa mkoani Mwanza watashuhudia baadhi ya michezo ya soka chini ya miaka 21 pamoja na fainali ya Ndondo Cup na kutoa ushauri wa kitaalamu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.