RC MTANDA AKUTANA NA WATUMISHI NA KUHIMIZA UBUNIFU, UWAJIBIKAJI NA KUWAJALI WANANCHI
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo amekutana na watumishi wa Ofisi ya mkuu wa Mkoa, Wakurugenzi na Wakuu wa idara kutoka halmashauri zote nane na kusisitiza uwajibikaji wenye weledi, ubunifu kwenye ukusanyaji Mapato, Usimamizi wa Miradi na kusikiliza kero za wananchi.
Akizungumza na watumishi hao kwenye kikao kazi hicho kilichofanyika ukumbi wa Ofisi ya mkuu wa Mkoa, Mhe.Mtanda aliyetumia nafasi hiyo pia kujitambulisha ameweka bayana anataka kuona Halmashauri zikiongeza ubunifu wa vyanzo vya mapato ili Serikali iweze kuweka mipango imara ya maendeleo.
"Ndugu watumishi wenzangu tuna wajibu wa kutimiza ndoto za Rais Samia za kuona kasi ya maendeleo kwa wananchi, tukasimamie miradi na ikamilike kwa wakati," Mkuu wa mkoa.
Mkuu huyo wa mkoa aliyehamishiwa hivi karibuni kituo cha kazi Mwanza akitokea Mara,amesema yupo mbioni kuanza ziara wilayani akianzia Ukerewe lengo ni kusikia kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi.
Aidha amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kumuamini na kuahidi kufanya kazi kwa uaminifu,uadilifu na kuwatendea mema wananchi.
Ameongeza siku chache zilizopita amekutana na viongozi wa dini,wakuu wa wilaya wakishauriana mambo kadhaa ya kiutendaji na leo anakutana na watendaji wa shughuli za Serikali ambao ni watu muhimu katika kuwaletea maendeleo wananchi.
Akitoa neno la shukurani mara baada ya hotuba ya mkuu wa mkoa,Katibu Tawala wa mkoa wa Mwanza Bw.Balandya Elikana amesema maagizo yote yamepokelewa na kufanyiwa kazi.
"Mhe.mkuu wa mkoa nakuahidi tutakujibu kwa vitendo kwa uchapakazi bora na wenye tija kwa wananchi,hatuna shaka na uwajibikaji wako ambao utakuwa mfano kwetu sisi",Balandya.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.