RC MTANDA AMPONGEZA RAIS SAMIA KWA KUTOA FEDHA CHANJO ZA MIFUGO
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amemshukuru na kumpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kugharamia chanjo za mifugo nchini hususani Ng'ombe, Mbuzi, Kondoo na Kuku.
Ametoa pongezi hizo leo tarehe 20 Desemba, 2024 Ofisini kwake wakati akizungumza na Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mhe. Ashatu Kijaji aliyefika kusalimia kufuatia ziara yake ya kikazi Mkoani Mwanza baada ya uteuzi wa kuongoza Wizara hiyo alioupata hivi karibuni.
Mhe. Mtanda amesema wananchi wa Mkoa wa Mwanza wanajihusisha sana na shughuli za uvuvi na Ufugaji hivyo kwa msaada wa gharama za chanjo wafugaji wataongeza kipato na kukuza ufugaji kutokana na uwepo wa eneo la kutosha na rafiki kwa ufugaji.
Aidha, ametumia wasaa huo kuwataka Wakurugenzi wa Halmashauri kutenga bajeti kusaidia juhudi za wizara hiyo katika uvuvi wa kisasa mathalani mradi wa BBT kwenye uvuvi hususani ujenzi wa gati za kuegesha boti na kurekebisha barabara ziweze kupitika kurahisisha uvuvi.
Naye, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ashatu Kijaji amebainisha kuwa kuku milioni 140 watachanjwa bure huku ng'ombe milioni 19 wakitarajiwa kuchanjwa na wafugaji watachangia gharama kwani Serikali itatoa Tshs. 500 kwa ng'ombe mmoja na Tshs. 300 kwa Kondoo na Mbuzi.
Vilevile, ametoa wito kwa wakuu wa mikoa inayojihusisha na uvuvi kushirikiana na wizara kukomesha uvuvi haramu na kwenye kutekeleza hilo akabainisha kuwa wakamatwe viongozi wa shughuli hiyo haramu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.