RC MTANDA AMSHUKURU DKT. SAMIA KUANZISHA OFISI YA KANDA YA ZIWA YA KUDHIBITI NA KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha Ofisi ya kanda ya ziwa ya mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya na kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini.
Shukrani hizo amezitoa leo wakati alipokua akitoa salamu katika kilele cha maadhimisho ya Kitaifa ya siku ya kupiga vita dawa za kulevya duniani, maadhimisho yaliyofanyika leo Juni 30 2024, kwenye uwanja wa Nyamagana
Akitoa taarifa ya hali ya dawa za kulevya katika Mkoa wa Mwanza kuanzia mwaka 2018 hadi 2023, Mhe. Mtanda amesema jumla ya wananchi waliopatikana na dawa za kulevya aina ya bangi ni 1797, mirungi 294, dawa za kulevya (cocaine, heroine na nyingine) 51 na kufanya jumla ya dawa zote kuwa 2142.
"Takwimu hizi zinabainisha kwamba bishara na matumizi ya dawa za kulevya hapa Mkoani Mwanza ni kubwa na inahitaji msukumo mkubwa kutoka kwa Serikali pamoja na wadau mbalimbali ili kuendelea kupambana na wazalishaji, wasambaji na watumiaji wa dawa za kulevya".
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza kutokukubali matumizi ya dawa za kulevya kwani zinaharibu jamii, na kama tutashirikiana pamoja tunaweza kulikabili janga hili.
Kadhalika Mhe. Mtanda amesema Mkoa huo unaendelea kusimamia na kufuatilia kwa karibu miradi ya kimkakati na miradi yote inayoendelea kujengwa ili kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ubora na kwa kuzingatia thamani ya fedha (Value for Money).
Maadhimisho ya Kitaifa ya siku ya kupiga vita dawa za kulevya duniani yamehitimishwa leo Mkaoni Mwanza na kuhudhuliwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Chama cha Mapinduzi, Viongozi wa kimila, mashirika mbalimbali, wadau na wananchi huku mgeni rasmi akiwa ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb.).
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.