Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ameongoza mkutano wa uhamasishaji wa kisera kuhusu ukuzaji na uendelezaji wa ushoroba za kilimo, uliofanyika jijini Mwanza.

Mkutano huo umeandaliwa na Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ukiwa na lengo la kuimarisha mikakati ya pamoja ya kukuza sekta ya kilimo na mifugo katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ambayo ni Simiyu, Geita, Mwanza, Mara, Kagera na Singida.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Mhe. Mtanda amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa viongozi wa ngazi za mikoa na wilaya katika kusimamia na kutekeleza sera zinazolenga kuongeza tija katika uzalishaji, kuimarisha masoko na kuvutia uwekezaji katika sekta ya kilimo na mifugo.

Mkutano huo umewakutanisha Wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri kutoka mikoa hiyo, ambapo washiriki wamejadili mikakati ya kuboresha miundombinu ya kilimo, kuongeza thamani ya mazao na kuendeleza ushoroba za kimkakati kwa manufaa ya wananchi.

Mkutano huo umefanyika katika Ukumbi wa Adden Palace Hotel, na unatarajiwa kuwa chachu ya mageuzi ya sekta ya kilimo katika ukanda huo.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.