RC MTANDA APIGA GIA ANGANI ATANGAZA MOTISHA PAMBA JIJI IKISHIKA NAFASI ZA JUU LIGI KUU
Timu ya soka ya Pamba Jiji FC ambayo mzunguko wa lala salama ya ligi kuu imeingia na gia kubwa kwa kutoa dozi za ushindi kwa timu pinzani, sasa imetangaziwa dau nono endapo itamaliza ligi hiyo huku ikiwa imeshika nafasi za juu kuanzia ya tano hadi kumi.
Akizungumza na wachezaji wa Pamba Jiji mapema leo Ofisini kwake kabla ya timu hiyo kushuka dimbani kumenyana na Wagosi wa Kaya (Coastal Union), Mtanda amesema awali malengo yalikuwa msimu huu ni kuhakikisha wanabaki ligi kuu.
Ameongea kuwa, kutokana na mwendo mzuri walionao malengo ni kushika nafasi za juu na hilo linawezekana endapo watashinda mchezo dhidi ya Coastal Union na Mashujaa FC.
"Mkakati wa kupigania kubaki ligi kuu huo sasa tunaugeuzia kisogo, tuanze kupigania nafasi za juu na motisha nono itakuwepo tukishika nafasi ya tano au kumi,"amesisitiza Mtanda ambaye pia ni mlezi wa Pamba Jiji.
Amewakumbusha wachezaji hao kuongeza bidii kwa kila mchezo wao kwani lala salama ya ligi kuu ni ngumu na waepuke aina yoyote ya utovu wa nidhamu ambao utaigharimu timu.
"Epukeni kufanya madhambi dimbani na kupewa umeme (akimaanisha kadi nyukendu) hii itasabisha mzigo kwa timu kwa kumkosa mchezaji muhimu." Amesisitiza Mkuu wa Mkoa.
Katika mazungumzo hayo Mtanda amewakabudhi wachezaji hao Tshs. milioni 11 mchango aliopewa na wadau wa soka walioamua kumchangia na kubaki milioni 4 ili zikamilike milioni 15 ahadi aliyowapa wachezaji hao ya shs milioni 30 baada ya ushindi wao dhidi ya Azam FC,awali aliwakabidhi milioni 15.
Katika mpambano wake wa leo uliopigwa dimbani CCM Kirumba Wana TP Lindanda wamezidi kuwasha endiketa kuelekea nafasi za juu katika msimamo wa ligi kuu baada ya kuwachezesha ngoma ya Mdumange timu ya Coastal Union kutoka Tanga kwa kuwabugiza mabao 2-0.
Kwa ushindi huo timu hiyo sasa imekwaa hadi nafasi ya 8 na mtaji wa pointing 21 kibindoni huku ikijiandaa na safari ya Kigoma kuwafuata Mashujaa FC mchezo utakaopigwa siku ya Jumatano Februari 19 kwenye uwanja wa Lake Tanganyika.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.