RC MTANDA ASHIRIKI HAFLA YA UVISHAJI NISHANI MAAFISA, WAKAGUZI NA ASKARI POLISI
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura leo 24 Mei, 2024 amewavisha nishani Maafisa, Wakaguzi, na Askari wa vyeo mbalimbali kutoka Mikoa ya Kanda ya ziwa kwenye Viwanja vya FFU Jijini Mwanza.
Akizungumza kwenye hafla hiyo IGP amewataka Jeshi la polisi kusimamia maelekezo ya kijinai kwani ndio dira ya utendaji kazi wa jeshi hilo na akawataka kusimamia utendaji kazi kuanzia ngazi za chini.
"Tutengeneze madawati ya ufuatiliaji na tathmini ya maelekezo kuanzia ngazi za juu hadi chini kwa ajili ya kuleta uelewa kwa askari mmoja mmoja kwani italeta urahisi kuratibu na kusimamia." IGP Wambura.
Aidha, amemshukuru Rais Samia kwa kuruhusu uvishaji nishani lakini pia upandishaji wa Madaraja kwa maafisa na askari wa jeshi hilo kwani kwa muda mrefu walikosa fursa na ujenzi wa makazi ya Askari na Maafisa na ameonesha kufurahishwa na maendeleo hayo huku akitamani jeshi hilo kuwa la mfano duniani.
Akitoa salamu za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametoa pongezi kwa jeshi hilo kwa kuimarisha amani nchini kwa kusimamia weledi kwenye kazi hasa nidhamu inayosaidia utulivu wa raia.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza kushirikiana na jeshi hilo na majeshi mengine nchini kuimarisha usalama kwenye makazi yao kwani Jeshi hilo limejitoa kuhakikisha wanawalinda raia na mali zao ili wawe huru kufanya shughuli za kujiletea maendeleo.
"Hongereni sana kwa kuvishwa nishani, nataka niwaambie kuwa taasisi yotote ni lazima isimamie haki, ijiepushe na matendo ya kuharibu maadili na haki kwa jamii, askari wote nataka mjenge heshma yenu wenyewe na ya jeshi letu makini." RC Mtanda.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa ametumia wasaa huo kuwapongeza wote waliovishwa nishani na ameishukuru Ofisi ya Mkoa wa Mwanza kwa ushirikiano wanaolipatia jeshi hilo kila wakati.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.