RC MTANDA ATAKA ADHABU KWA WANAFUNZI IZINGATIE MIONGOZO YA ELIMU
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka Walimu Mkoani humo kutoa adhabu kwa wanafunzi kulingana na miongozo na sheria za nchi ili kujenga tabia ya ushirikiano na umoja baina ya wazazi na walimu.
Amesema hayo leo ijumaa tarehe 20 Septemba 2024 wakati akizungumza na wazazi na wanafunzi wa shule za Blessing modal wakati wa mahafali ya wanafunzi wa darasa la saba na awali.
Aidha, ameupongeza uongozi na walimu wa shule hiyo kwa mafanikio wanayoyapata mwaka hadi mwaka mpaka kufikia hatua ya kufaulisha kwa daraja A kwenye masomo na kupelekea wazazi kuwapeleka watoto wao hata kuzidi elfu moja tofauti na wanafunzi 8 tu wakati inaanzishwa.
Vilevile, amewapongeza kwa kulinda tamaduni, miiko, desturi, silka na mila za kitanzania na kuwalea watoto kwenye maadili safi kwa kuwakuza kwenye miongozo ya kidini bila ubaguzi wala upendeleo wa upande mmoja.
"Nimefurahishwa sana na onesho lililofanywa hapa na nimeamini hapa hata kama shule haina dini lakini mnazingatia imani za wanafunzi wenu, na mnawafundisha hata kupika nimependezwa sana". Amesema Mkuu huyo wa Mkoa.
Akizungumzia maadili, Mhe. Mtanda amewataka wazazi kushirikiana na walimu wanaowalea watoto wakati wawapo shuleni na kuwa na mawasiliano ya karibu na shule ili kusimamia kwa pamoja makuzi ya watoto.
"Msiwaache watoto wakajilea wenyewe au kwa msaada wa wafanyakazi, mtapoteza upendo kwa watoto wenu hakikisheni mnatenga muda kwa watoto ili mtengeneze mapenzi na watoto wenu".
Vilevile, ametumia jukwaa hilo kutoa wito kwa jamii kulinda amani nchini ili wananchi waendelee kuwa na utulivu wakati wanaendelea na majukumu yao ya kujipatia kipato hususani kwenye kilimo, uvuvi, uchimbaji wa madini na biashara.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.