Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka wazazi na walezi mkoani humo kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wa kuwanunulia watoto vifaa muhimu vya masomo na kuwapeleka shuleni mara moja bila kuchelewa.

Agizo hilo limetolewa wilayani Kwimba wakati Mkuu wa Mkoa alipokuwa akikagua ujenzi wa madarasa sita na matundu 18 ya vyoo katika Shule ya Awali na Msingi Ilula miradi inayotekelezwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 195.3.

Katika ziara hiyo Mhe. Mtanda alibaini hali duni ya uripoti wa wanafunzi ambapo ni wanafunzi 51 pekee kati ya 150 walioandikishwa ndio walioripoti shule.

Kutokana na hali hiyo Mhe. Mtanda amewaagiza wenyeviti wa vijiji na mitaa kuhakikisha wanapiga mbiu na kuwakumbusha wazazi na walezi kuwapeleka watoto shuleni akisisitiza kuwa muhula wa masomo tayari umeanza tangu mwanzoni mwa juma.

“Ninawaagiza wazazi na walezi watimize wajibu wao wa kuwanunulia watoto vifaa muhimu vya masomo na wenyeviti wa vijiji na mitaa wahakikishe wanapiga mbiu ya kuwakumbusha wazazi kuwapeleka watoto shuleni mara moja, kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa,” alisema Mhe. Mtanda.

Aidha Mkuu wa Mkoa ametoa katazo kwa walimu wakuu na wakuu wa shule kutoanzisha au kutochangisha michango yoyote isiyo na miongozo utaratibu au ambayo haijapitishwa na mamlaka halali akibainisha kuwa vitendo hivyo huwakwamisha wanafunzi na kuwanyima haki yao ya kupata elimu bila vikwazo.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.