RC MTANDA ATOA MUDA WA MIEZI MITATU WANAODAIWA 5% YA MIKOPO YA HALMASHAURI KUZIREJESHA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka wanachi wote wanaodaiwa marejesho ya mikopo waliyochukua kutoka Halmashauri ya wilaya ya Magu zaidi ya mil. 148 kuhakikisha wanazirejesha fedha hizo ndani ya miezi mitatu ili na wananchi wengine wenye sifa na vigezo waweze kunufaika.
Mhe. Mtanda ametoa kauli hiyo mapema leo Juni 28, 2024 alipokuwa akizungumza katika kikao cha Baraza Maalumu la Madiwani cha kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) za mwaka 2022/2023 na kuipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Magu kwa kupata hati inayoridhisha na ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
"Mkopo huu sio hisani na wala sio mgao wa kula, wale wote waliopitiliza muda wa marejesho watafutwe wabanwe wazilipe ili tuweze kuwakopesha wanawake wengine, nchi hii ina wahitaji wengi".Mtanda
Mkuu huyo wa Mkoa amesema nia ya Serikali kutoa 5% ya fedha ya mapato ya ndani za Halmashauri ni kuwasaidia wanawake katika harakati za kupambana na kujikomboa na umaskini kwa kuwawezesha kutumia fedha hizo katika kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo.
Aidha Mhe. Mtanda ameitaka Halmashauri hiyo kuhakikisha wanamaliza hoja 11 zilizobakia kwa wakati na kusema kuwa ameridhishwa na namna walivyojipanga kuzimaliza hoja hizo. Kadhalika amewataka kuwasilisha Mkoani mpango kazi wa namna ya kuzimaliza hoja hizo ifikapo tmJunu 29,2024 mwaka huu ili mpango kazi huo uunganishwe na utumwe Wizarani TAMISEMI.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Mhe. Simon Pandarume amesema wao kama Halmashauri wana ushirikiano wa kutosha kwani wamefanikiwa kuongeza mapato ya ndani kutoka sh. bil. 2.4 na kufikia bil. 4.4 kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
"Tumefungua Shule nyingi kwa mapato ya ndani, 19 mpya za Sekondari na 7 za Msingi kwa miaka minne, tumepeleka pia fedha nyingi kwenye zahanati, nyumba za watumishi, wakiwemo waalimu". Amesema Mhe. Pandarume.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.