RC MTANDA ATOA SIKU 7 KWA WAKUSANYA USHURU MAGU KUWASILISHA FEDHA BENKI
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametoa muda wa Siku 7 kwa watumishi wanaokusanya mapato kwenye halmashauri ya Wilaya ya Magu kuhakikisha wanawasilisha fedha zaidi ya Tshs. Milioni 15 benki na wasipotekeleza hayo watawachukulia hatua za sheria.
Mhe. Mtanda ametoa agizo hilo leo Juni 13, 2024 wakati akizungumza na baadhi ya wazee, wadau wa maendeleo pamoja na watumishi wa Halmashauri na kubaini kuwa Halmashauri hiyo imekusanya mapato ya ndani kwa 87% tu kwa mwaka unaoishia Juni 30, 2024.
"Halmashauri yenu haifanyi vibaya lakini haijafikia malengo ya ukusanyaji wa wapato ya ndani, naelekeza siku chache zilizobakia halmashauri ifikishe asilimia mia na kwa wanaodaiwa zaidi ya milioni 15 ndani ya siku 7 wawasilishe benki fedha hizo." Mkuu wa Mkoa.
Mtanda amefafanua kuwa ili kutekeleza jambo hilo ni lazima kuwe na uzingatiaji wa sheria kwenye ukusanyaji pamoja na matumizi ikiwemo upelekaji wa fedha za mapato ya ndani kwenye miradi ya maendeleo ili wananchi wapate huduma za kijamii zilizoboreshwa.
Mhe. Joshua Nathari, Mkuu wa Wilaya ya Magu amesema hawajafika lengo la makusanyo ya mapato ya ndani kwani wamekusanya Tshs. Bilioni 3.7 ambayo ni asilimia 87 ya makadirio na kwamba wameweka mkakati wa kuzifikia 92 za kisheria za OR -TAMISEMI kupitia chanzo cha Stendi ya Kisesa.
Ameongeza kuwa, kwa mwaka 2023/24 wamepokea fedha nyingi za kutekeleza miradi ya maendeleo katika sekta za Afya, Elimu, Ardhi, kilimo, Miundombinu na kwamba nishati ya umeme imefika kwenye vijiji vyote (Gridi ya Taifa) kasoro kimoja tu na usambazaji maji inaridhisha sana.
Aidha Mhe. Mtanda amewataka wataalamu wa afya kuhakikisha wanasimamia uwepo wa madirisha ya wazee kikamilifu kwani sera ya nchi inaelekeza wazee watibiwe bure na wasitozwe chochote.
"Nataka kutoa onyo kwa wataalamu wa afya wanaowahudumia wazee na mwisho wa matibabu wanawaambia wakanunue dawa, ni marufuku kufanya hivyo kwani mnachotakiwa ni kukamilisha matibabu yao kwani Serikali inagharamia na tuweke madirisha maalumu kwa ajili yao." Amesisitiza Mkuu wa Mkoa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.