Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametoa siku 90 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba kuhakikisha inapeleka fedha za ukamilishaji wa ujenzi wa Vituo vya Afya vya Isunga na Kikubiji akisisitiza kuwa hatavumilia uzembe katika miradi ya maendeleo.

Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Isunga baada ya kukagua ujenzi wa majengo ya huduma za afya ulioanza mwaka 2021 Mhe. Mtanda amesema kucheleweshwa kwa ukamilishaji wa miradi hiyo ni dalili ya kutowajibika kwa baadhi ya viongozi wa halmashauri husika.

Amesema Serikali Kuu tayari imetoa shilingi milioni 500 kwa ajili ya Kituo cha Afya Isunga, lakini Halmashauri imetoa shilingi milioni 40 pekee kati ya shilingi milioni 90 zilizotakiwa kuchangia kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi huo.

“Nitatumia jitihada zangu zote kuhakikisha miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Mwanza inakamilika kwa wakati. Mkuu wa Wilaya simamia suala la kuletwa kwa fedha hizi, na ndani ya siku 90 nipate taarifa ya kukamilika kwa mradi huu pamoja na kituo cha Kikubiji.” amesema Mhe. Mtanda.

Ameeleza kuwa kukamilika kwa vituo hivyo kutawawezesha wananchi zaidi ya 4,061 kupata huduma bora za afya ikiwemo huduma za mama na mtoto, upasuaji, maabara pamoja na huduma za wagonjwa wa nje.

Katika hatua nyingine Mhe. Mtanda amewataka wataalamu wa afya kushirikiana na viongozi kuanzia ngazi ya vitongoji kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote, ili kuongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa gharama nafuu.

Amesisitiza kuwa elimu hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya siku 100 za Serikali ya Awamu ya Sita yenye lengo la kuboresha huduma za kijamii na kuongeza ustawi wa wananchi.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.