Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa dhamira ya dhati miongoni mwa wajumbe wa Kamati ya Maadhimisho ya Sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026 Kitaifa kutoka Mkoa wa Rukwa, akibainisha kuwa dhamira ndiyo nguzo kuu ya mafanikio ya tukio lolote la kitaifa.

RC Mtanda ametoa msisitizo huo wakati wa mazungumzo na wajumbe hao waliotembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa lengo la kujifunza na kupata uzoefu wa maandalizi ya Sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa zitakazofanyika Mkoani Rukwa tarehe 14 Oktoba, 2026.

Akizungumza kwa niaba ya Kamati hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa Bw. Msalika Robert Makungu amesema wajumbe wa kamati wamegawanyika katika makundi mawili, kundi moja likitembelea Mkoa wa Manyara na lingine likiongozwa na yeye mwenyewe likitembelea Mkoa wa Mwanza kwa lengo la kujifunza namna ya kuandaa na kusimamia sherehe za Kuzima Mwenge wa Uhuru.

RC Mtanda amesema kuwa ili sherehe za kitaifa zifanikiwe ni lazima kuzingatia mambo muhimu ikiwemo ushiriki wa wananchi kwa wingi, upangaji wa bajeti ya kutosha, urembo wa tukio kupitia matangazo na sare zinazovutia pamoja na uwepo wa mfumo mzuri wa uratibu na uendeshaji wa shughuli.

Ameongeza kuwa vikao vya kupanga na ushirikishwaji wa wadau ni muhimu ili kuhakikisha kila mmoja anakuwa na uelewa wa majukumu yake.

Akihitimisha, amewahimiza wajumbe wa Kamati ya Maadhimisho ya Mwenge wa Uhuru 2026 Mkoa wa Rukwa kujitoa kwa moyo wote, akisisitiza kuwa kujituma hakufundishwi bali hutokana na dhamira binafsi na ushirikiano wa pamoja.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.