Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba leo tarehe 23 Januari, 2026 amezindua rasmi meli mpya ya kisasa ya Mv. New Mwanza iliyojengwa na Mkandarasi Gas Entec Ship- Building kutoka Korea kwa gharama ya Tshs. Bilioni 120.56.

Akizungumza na wananchi katika eneo la Bandari ya Mwanza Kusini Mhe. Waziri Mkuu amesema kuwa ujenzi wa Meli hiyo ya kisasa ni ishara ya juhudi za serikali kuwaletea maendeleo wananchi kwa kuhakikisha wanamaliza kiu ya kuwa na usafiri imara katika ziwa Victoria.

Aidha, ameiagiza Wizara ya Uchukuzi kuendeleza ujuzi uliotumika kujenga meli hiyo, TASHICO washirikiane na wadau wengine kulinda mradi huo kwa kuweka bima na kufuata ushauri wa kitaalamu na kuimarisha na kukuza diplomasia ya mahusiano na amani.

Halikadhalika, ameziagiza wizara zinazosimamia miradi ya maendeleo mathalani miundombinu kufanya tathmini kubaini miradi ambayo wakandarasi hawajalipwa fedha ili walipwe na ikamilike kama mradi huo wa meli na kuleta tija kwa jamii.

“Naomba niwaagize Mawaziri wa kisekta, fanyeni tathmini kwenye miradi yote ambayo mikataba imeshasainiwa lakini wakandarasi hawajapata fedha za awali na wizara ya fedha pitieni mafungu yote isipokuwa ya vyombo vya usalama na Afya mkate mpeleke fedha kwenye miradi hii ili ikamilike.” Waziri Mkuu.

“Wakati serikali ya awamu ya sita inaingia madarakani ilikuta meli hii imejengwa kwa 40% zikiwa zimelipwa Tshs. Bilioni 40.64 tu, tunamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kulipa Tshs. Bilioni 79.98 na kuwezesha mradi huu kukamilika.” Amesema Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa.

“Meli hii itaboresha utoaji na upatikanaji wa huduma kwa wananchi, mathalani kupunguza adha za usafiri kwa wananchi walizokuwa wakizipata au kupeleka bidhaa zao nje ya Mwanza kama vile Mkoa wa Kagera na Nchi Jirani za Kenya na Uganda.” Amesema Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.